Ranieri: Ndoto yangu ya Leicester 'imekufa'

Aliyekuwa kocha wa Leicester asema ndoto yake ya leicester imekufa baada ya kufutwa kazi

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Aliyekuwa kocha wa Leicester asema ndoto yake ya leicester imekufa baada ya kufutwa kazi

Aliyekuwa mkufunzi wa klabu ya Leicester Claudio Ranieri amesema kuwa ndoto yake imepotea wakati alipopigwa kalamu kama kocha wa klabu hiyo miezi tisa baada ya kuisaidia kushinda taji la ligi.

Ranieri mwenye umri wa miaka 65 aliiongoza Leicester kushinda taji hilo licha ya kuorodheshwa kuwa na nafasi moja kati ya 5000 kushinda taji hilo.

Leicester sasa iko pointi moja juu ya eneo la kushushwa daraja huku ikiwa imesalia mechi 13.

''Baada ya furaha ya mwaka uliopita na kushinda taji la ligi nilikuwa na ndoto ya kusalia na Leicester.Kwa bahati mbaya haikuwezekana''.

''Fursa hiyo ilikuwa nzuri na itakuwa nami maishani''.

''Ninamshukuru kila mtu katika klabu hiyo,kila mtu aliyeshiriki katika ufanisi ,hususan mashabiki''.

''Muliniweka katika nafsi zenu kuanzia siku ya kwanza na kunipenda.Ninawapenda nyie pia nami''.

''Hakuna mtu anayeweza kuchukua kile tulichofanikiwa kupata pamoja na natumai munalifikiria hilo na kutabasamu kila siku ninavyotabasamu''.