Yanga yamaliza hasira kwa Ruvu Shooting

Yanga-Tanzania Haki miliki ya picha Google
Image caption Furaha ya bao , Simon Msuva

Baada ya kuchapwa na watani wao wa jadi Jumamosi iliyopita, mabingwa watetezi wa taji la ligi kuu Tanzania bara Yanga Sports Club, wameibukia kwa Ruvu Shooting na kuitandika magoli 2-0 kwenye mechi yao ya kiporo iliyochezwa uwanja wa taifa.

Goli la kwanza la Yanga lilipatikana kwa mkwaju wa penati baada ya beki wa Ruvu Shooting kuushika mpira akiwa kwenye eneo la hatari. Mpigaji wa penati wa Yanga Simon Msuva akakwamisha mpira kambani na kuiandikia Yanga bao la kuongoza.

Jambo lililozua utata kwenye mchezo huo ni pale mwamuzi wa mchezo Ahmad Simba alipolikataa goli la Obrey Chirwa na kumuonesha kadi ya njano kwa madai alifunga goli hilo kwa mkono. Chirwa alifunga goli hilo kwa kichwa akiunganisha krosi ya Simon Msuva kutoka Kusini Magharibi ya uwanja.

Dakika chache baadaye, mwamuzi akamuonesha Chirwa kadi ya pili ya njano iliyosababisha kadi nyekundu kwa kuudundisha mpira akiashiria kutokubaliana na maamuzi ya refa aliyepuliza filimbi baada ya Chirwa kumfanyia faulo mchezaji wa Ruvu Shooting.

Kipindi cha pili Yanga wakiwa pungufu walipoteza nafasi kadhaa za kufunga lakini nafasi zitakazokumbukwa zaidi ni zile za Msuva na Tambwe.

Wakati mechi inaelekea ukingoni, Emanuel Martin aliyeingia akitokea benchi, aliifungia Yanga bao la pili na la ushindi kwa kichwa alipounganisha pasi ya Musuva na kumwacha golikipa wa Ruvu Shooting Bidii Hussein akiwa hoi baada ya kujaribu kuufuata mpira na kujigonga kwenye nguzo ya goli.

Yanga imefikisha pointi 52 pointi mbili nyuma ya Simba huku timu zote zikiwa zimeshacheza mechi 23 hadi sasa, Yanga inaendelea kusalia katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kuu Tanzania bara huku Simba wakiendelea kusalia vinara wa kwenye msimamo.