Manchester United kukabili Chelsea bila Rooney na Ibrahimovic

Wayne Rooney Haki miliki ya picha PA
Image caption Wayne Rooney ni miongoni mwa wachezaji wanane waliofungia United mabao katika Kombe la FA msimu huu

Nahodha wa Manchester United Wayne Rooney hataweza kuchezea klabu hiyo wakati wa mechi ya robo fainali Kombe la FA dhidi ya Chelsea uwanjani Stamford Bridge Jumatatu usiku. Mechi hiyo itachezwa saa tano kasorobo saa za Afrika Mashariki.

Rooney aligongana na Phil Jones wakifanya mazoezi na akaumia mguuni.

Mshambuliaji mwingine wa United Zlatan Ibrahimovic atakuwa anaanza kutumikia marufuku ya kutocheza mechi tatu, adhabu aliyopewa kwa kumgonga Tyrone Mings wa Bournemouth kwa kiwiko cha mkono.

Washambuliaji wengine wa United Anthony Martial na Marcus Rashford wanaugua na hawataweza kuchezea mashetani hao wekundu.

Kikosi cha Antonio Conte kiko shwari bila wachezaji wowote kutatizwa na majeraha au kupigwa marufuku.

Conte amesema ni wazi kwamba Manchester United na Manchester City ndio wenye vikosi vya wachezaji stadi zaidi Ligi Kuu ya Uingerez na hivyo basi anatarajia upinzani mkali.

"Ningependa kuangazia zaidi mechi na wachezaji wangu," amesema.

Meneja wa United Jose Mourinho, ambaye wachezaji wake walisafiri Urusi kwa mechi ya Ligi ndogo ya klabu Ulaya, Europa League, Alhamisi wiki iliyopita, amesema Manchester United hawababaishwi na Chelsea licha ya wasiwasi kwamba huenda wachezaji wake wakatatizwa na uchovu.

"Manchester United ni klabu kubwa. Manchester United ndiye bingwa wa michuano hii.

"Si makosa ya Chelsea kwamba tulipangiwa kucheza mechi hii Jumatatu, kwa hivyo ni wazi kwamba tutafanyia kikosi chetu mabadiliko ... lakini hatuwezi kwenda Stamford Bridge na timu ya Nicky Butt (wachezaji wasiozidi umri wa miaka 23).

Haki miliki ya picha Getty Images

Ni mara ya 12 kwa United na Chelsea kukutana Kombe la FA. Katika mechi 11 za awali, United wameshinda mechi nane na Chelsea tatu.

Blues hata hivyo walishinda mechi zote mbili zilizokutanisha timu hiyo mbili Kombe la FA mwongo huu, wakishinda 1-0 fainali 2007 na pia raundi ya sita uwanjani Stamford Bridge mwaka 2013 walipoibuka na ushindi wa 1-0.

Chelsea hawajashindwa mechi 11 walizocheza karibuni ligini na katika vikombe dhidi ya United (wameshinda sita na kutoka sare tano), na wamefungwa mara tatu pekee katika mechi tisa za karibuni zaidi.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii