Paul Pogba: Kiungo wa kati wa Manchester United apata jeraha

Paul Pogba Haki miliki ya picha PA
Image caption Pogba aliondoka uwanjani kwa kuchechemea kipindi cha pili

Kiungo wa kati wa Manchester United Paul Pogba hataweza kuchezea klabu hiyo mechi ya Ligi ya Premia Jumapili ugenini dhidi ya Middlesbrough.

Hii ni baada yake kupata jeraha kwenye misuli ya paja.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa aliumia kipindi cha pili cha mechi ya ligi ndogo ya klabu Ulaya, Europa League, kati ya United na FC Rostov ya Urusi na ikamlazimu kuondoka uwanjani.

Nafasi yake ilijazwa na Marouane Fellaini.

Manchester United walishinda 1-0 kupitia bado la Juan Mata na wakasonga hati robofainali kwa ushindi wa jumla wa 2-1 dhidi ya Rostov.

Pogba, 24, pia anatarajiwa kukosa pia mechi za timu ya taifa ya Ufaransa dhidi ya Luxembourg na Uhispania baadaye mwezi huu.

Haki miliki ya picha Getty Images

Meneja wa United Jose Mourinho hakusema Pogba anatarajiwa kukaa nje muda gani.

Alipoulizwa iwapo huenda ikawa karibu wiki tatu, Mourinho alisema: "Kweli. Lakini sina uhakika, lakini kwa kweli hawezi kucheza dhidi ya Middlesbrough na hatachezea timu ya taifa."

Pogba ndiye mchezaji aliyenunuliwa ghali zaidi duniani na amefungia United mabao saba na kusaidia ufungaji wa mengine matano katika mechi 41 alizowachezea msimu huu.

Mholanzi Daley Blind pia alilazimika kuondoka uwanjani kutokana na kilichoonekana kuwa jeraha lililotokana na kugongwa.

Hata hivyo, hali yake kamili haijaelezwa.

Mada zinazohusiana