Jose Mourinho alalamikia mechi ya Manchester United na Middlesbrough

Paul Pogba Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Kiungo wa kati wa Manchester United Paul Pogba hatacheza dhidi ya Middlesbrough

Meneja wa Manchester United amesema anaamini wasimamizi wa Ligi Kuu ya Uingereza hawajali maslahi ya klabu za Uingereza zinazocheza ligi kuu za klabu Ulaya.

United watakutana na Middlesbrough Jumapili saa sita mchana saa za Uingereza.

Wataingia uwanjani saa 62 pekee baada ya kucheza mechi ya ligi ndogo ya klabu Ulaya, Europa League, Alhamisi ambayo walishinda FC Rostov hatua ya 16 bora.

Mourinho amesema una uwezekano mkubwa kwamba United watashindwa na kwamba inafaa kuwa jambo la msingi kwamba mechi hiyo ilifaa kuanza saa kumi na moja jioni.

"Hawajali hata kidogo," aliongeza Mreno huyo kuhusu wasimamizi wa Ligi ya Premia.

Huwa kuna makubaliano kwamba klabu ambazo zinacheza mechi Europa League hazipangiwi kucheza Jumamosi.

Hali kwamba kutakuwa na mapumziko ya kimataifa baada ya mwisho wa wiki imeifanya mechi hiyo ya United na Middlesbrough kutochezwa Jumatatu.

Watangazaji wa mechi za Ligi ya Premia Sky na BT Sport huamua ni mechi gani watatangaza moja kwa moja kwenye runinga.

Sky wanaweza kuonesha mechi mbili za adhuhuri Jumapili ambazo zitakuwa - Tottenham v Southampton na Manchester City v Liverpool wikendi hii.

Mechi hiyo ya Middlesbrough itatangazwa na BT Sport, ambao huwa wanaweza kuonesha mechi ya saa sita.

Mourinho amesema wasimamizi wa soka mataifa mengine huwa wanasaidia zaidi klabu zinazocheza Ulaya.

"Nchini Italia, klabu zinazofika hatua ya muondoano na kucheza Jumanne au Jumanne, wiki ambayo imetanguliwa huwa wanacheza Ijumaa. Ureno, inayofuata, huwa wanapangiwa mechi zao Jumatatu," alisema.

Mourinho amesema anafahamu mkataba wa runinga wa jumla ya £10.4bn ndio unaopewa kipaumbele.

"Ni kwamba wanaambia 'huwa tunawapa pesa nyingi sana,'" alisema.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii