Manchester United yamruhusu Bastian Schweinsteiger kujiunga na Chicago Fire

Bastian Schweinsteiger Haki miliki ya picha PA
Image caption Bastian Schweinsteiger

Manchester United imekubali kamuachia kiungo wake wa kati Bastian Schweinsteiger, ili apate kujiunga na Chicago Fire.

Makubaliano kati ya vilabu hivyo yaliafikiwa siku ya Jumatatu, na sasa yuko kwenye harakati za kufanyiwa uchunguzi wa kiafya na kupata visa.

Nahodha huyo wa zamani wa kikosi cha Ujerumani mwenye umri wa miaka 32, ametia sahihi mkataba wa mwaka mmoja kwa mujibu wa gazeti la Tribune la Chicago.

"Nina huzuni kwa kuwaacha marafiki zangu wengi huko Manchester United, lakini ninatoa shukran kwa klabu yangu kwa kuniruhusu kuchukua jukumu hilo, Alisema Schweinsteiger.

Schweinsteiger, ambaye aliiongoza Ujerumani kushinda kombe la dunia mwaka 2014, alifanya mazungumzo na Chicago fire mwaka uliopita, lakini akaamua kusalia Manchester United hata baada ya msimu wa kuhama kukamilika.

Wiki ijayo alifanya mazoezi na timu ya vijana ya Machester United wakati wanajiandaa kwa mechi ya Europa League dhidi ya FC Rostov.

Schweinsteiger, ambaye alijunga na Manchester United ikiwa chini na ukufunzi wa Louis van Gaal mwaka 2015, alifanya mazoezi na kikosi cha wachezaji wasiozidi miaka 23 wakati Jose Mourinho alichukua usukani msimu uliopita.