Arsene Wenger: Arsenal imesitisha mazungumzo na Sanchez na Ozil

Alexis Sanchez na Mesut Ozil Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Alexis Sanchez alijiunga na Arsenal 2014, mwaka mmoja baada ya Mesut Ozil

Meneja wa Arsenal Arsene Wenger amesema klabu hiyo imesitisha kwa muda mazungumzo kuhusu mikataba ya Alexis Sanchez na Mesut Ozil hadi mwisho wa msimu.

Mshambuliaji wa Chile Sanchez na kiungo wa kati wa Ujerumani Ozil, wote wenye umri wa miaka 28, wamesalia na chini ya miaka miwili kwenye mikataba yao.

Wenger amesema tayari amefanya uamuzi wake kuhusu mustakabali wake Arsenal, lakini bado hajatia saini mkataba wa miaka miwili aliopewa na klabu hiyo.

"Kwa sasa hatujaafikiana," Wenger alisema kumhusu Sanchez.

Akiongea na BeIn Sports, Mfaransa huyo wa umri wa miaka 67 alisema: "Tumeamua kuangazia mwisho wa msimu na tuandae mazungumzo majira ya joto.

"Hali ni sawa kwa Ozil, kwa sababu unapokosa kupata makubaliano na mashauriano bado yanaendelea, hilo si jambo jema.

"Ni vyema kuketi na kuiangazia majira ya joto."

Haki miliki ya picha Rex Features

Arsenal wameshuka hadi nambari sita Ligi ya Premia baada ya kushindwa mechi nne kati ya tano walizocheza karibuni zaidi.

Kuhusu mustakabali wake, Wenger alisema: "Bila kujali nitasalia katika klabu hii muda gani bado nitabaki kujitolea na kuangazia kabisa (majukumu yangu) muda wote nitakaokuwa katika klabu hii."

Gunners watarejea uwanjani Ligi ya Premia Jumapili tarehe 2 Aprili watakapokuwa wenyeji wa Manchester City.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii