Mkenya Clifton Miheso adai kutishiwa kwa bunduki Afrika Kusini

Clifton Miheso
Image caption Miheso ameichezea timu ya taifa ya Kenya mechi 14 na kufunga magoli matano

Mchezaji wa kimataifa wa Kenya Clifton Miheso amewasilisha rasmi malalamiko katika shirikisho la soka duniani Fifa akidai kwamba alilazimishwa kwa mtutu wa bunduki kuhitimisha mkataba wake katika klabu ya Golden Arrows.

Miheso anadai kisa hicho kilitokea 14 Januari katika afisi za klabu hiyo mjini Durban nchini Afrika Kusini.

Mchezaji huyo wa miaka 24 anataka Golden Arrows wapigwe marufuku kununua au kuuza wachezaji au wapewe adhabu nyingine yoyote ile.

Aidha, anataka alipwe jumla ya $22,000 ambazo anasema anaidai klabu hiyo kama ujira wake.

Golden Arrows wamekanusha tuhuma za mchezaji huyo lakini wakakataa kuzungumzia zaidi kisa hicho.

Mwakilishi wa winga huyo anasema kalbu hiyo haikutoa maelezo yoyote ya kuridhisha kuhusu kisa hicho.

Miheso ameichezea timu ya taifa ya Kenya mechi 14 na kufunga magoli matano.

Mada zinazohusiana