Peter Odemwingie ajiunga na klabu ya Indonesia

Peter Odemwingie
Image caption Peter Odemwingie

Mshambuliaji wa zamani wa Nigeria Peter Odemwingie amesema angependa kucheza kama alivyokuwa hapo awali kwa kufunga mabao muhimu baada ya kujiunga na klabu ya Madura United

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 35 aliyeichezea timu ya taifa ya Nigeria Super Eagles katika mashindano ya kombe la dunia mwaka 2010 na 2014 ametia saini mkataba wa mwaka mmoja ambao waweza kuongezwa.

Mchezaji huyo wa zamani wa Westbrom na Stoke City alikuwa akiichezea Rotherham lakini akaondoka Januari.

"Huu ni wakati mzuri sana katika soka nchini Indonesia na nina furaha kushiriki," aliiambia BBC Spoti.

"Nina matumaini nitaifungia Madura mabao muhimu."

Odemwingie ni mchezaji wa tatu wa zamani wa ligi kuu ya Uingereza kuhamia Indonesia baada ya Michael Essien na Carlton Cole.

"Sikuwa na habari yoyote kuhusu jinsi mambo yalivyo hapa lakini nimezungumza na Michael Essien ambaye amenieleza mambo ni mazuri," Odemwingie alieleza.

Kutambulika kama mchezaji muhimu sio jambo dogo, nimechezea nchi kadhaa za Uingereza lakini hapa panavutia sana, na watu wana roho nzuri.