Claudio Ranieri anasema alichochewa na mtu katika klabu lakini sio wachezaji

Aliyekuwa meneja wa Leicester Claudio Ranieri

Chanzo cha picha, AP

Maelezo ya picha,

Claudio Ranieri anasema alichochewa na mtu katika klabu lakini sio wachezaji

Meneja wa zamani wa Leicester Claudio Ranieri anaamini kuwa kuna mtu kwenye klabu aliyekuwa anampinga lakini anasema hadhani ni wachezaji waliosababisha yeye kupigwa kalamu.

Muitaliano huyo aliongoza klabu ya Leicester kushinda ligi kuu msimu uliopita lakini akafutwa Februari.

"Siwezi kuamini kuwa ni wachezaji wangu walionimaliza, hapana,hapana," aliwaeleza wanahabari wa spoti wa Sky "

"Labda ni mtu mwingine tu. Nilikuwa na tatizo kidogo mwaka uliopita na tulishinda ligi. Labda mwaka huu tutakaposhindwa, watu watatia bidii kiasi."

Wakati Ranieri alifutwa kazi Leiceter ilikuwa pointi moja juu ya eneo la kushushwa ngazi la ligi kuu.

Meneja msaidizi Craig Shakespeare alipewa kazi yaa kuifunza timu hiyo na kuiongoza kushinda mechi tano za ligi kuu.

"Mimi husikiza mambo mengi sana," alisema Ranieri huku akikataa kusema aliyekuwa anazungumzia.

"Sitaki kusema ni nani. Mimi ni mwaminifu. Kile nilichokuwa nacho nilikisema uso kwa uso."