Wenger hataki kuzungumzia hatma yake ndani ya Arsenal

Wenger 'hayuko tayari' kujadili hatma yake ya baadaye

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Wenger 'hayuko tayari' kujadili hatma yake ya baadaye

Mkufunzi mkuu wa timu ya Arsenal, Arsene Wenger, anasema kuwa hatma yake ya baadaye "haitawatatiza kwa vyovyote wachezaji."

Aidha, Wenger anakiri kuwa mabao 3-0 waliotingwa na timu ya Crystal Palace ni "jambo la kuleta wasiwasi mkubwa".

Kandarasi ya Wenger inamalizika mwishoni mwa msimu huu, huku akikabidhiwa kandarasi mpya ya miaka mingine miwili, ingawa hajatangaza iwapo ataendelea kuifunza Arsenal au la.

Arsenal iliyo katika nafasi ya 6, iko na alama saba nyuma ya timu nne zilizoko katika nafasi za kwanza, huku ikisalia na mechi nane tu kukamilisha msimu huu.

"Nimeiongoza Arsenal katika mechi 1,100, na hatujawahi kushindwa namna hii," amesema mfaransa huyo.

"Ilibidi tujibu mara moja, lakini hatujakubali."

Maelezo ya picha,

Masaibu ya Arsenal kwenye gazeti la The Sun

Baadhi ya mashabiki wamemuambia Wenger, muda "umefika wa kuondoka", huku pia wakiimba, "haufai kuvalia shati hilo" baada ya Arsenal kupata kichapo cha mbwa na timu ya Palace iliyo katika hatari ya kushushwa daraja.

Mabao kutoka kwa Andros Townsend, Yohan Cabaye na Luka Milivojevic, iliongeza uchungu kwenye jeraha la Arsenal ya kupata kichapo mara nne mfululizo ya mechi ya ugenini- kwa mara ya kwanza chini ya ukufunzi wa Wenger wa misimu 21.

Hii inawaacha washikaji bunduki, katika hatari kubwa ya kukosa kufikia timu nne bora zitakazomaliza msimu huu, kwa mara ya kwanza katika historia ya miaka 67 iliyopita.

"Naelewa namna mashabiki wetu waIivyokata tamaa, nasi pia tumetamaushwa mno," alisema.

"Ni jambo la kutia wasiwasi na kukatisha tamaa, jinsi tulivyopoteza mechi hii. Wachezaji wa Crystal Palace walikuwa wakakamavu, waliicharaza Chelsea hivi majuzi, na hiyo inaonesha bayana kuwa ni wachezaji bora.

"Tuko katika hali mbaya. Mechi hii haijasaidia chochote." Alisema Arsene Wenger.