Mourinho: Manchester United waliwadhibiti Chelsea

Jose Mourinho and Antonio Conte

Chanzo cha picha, Rex Features

Maelezo ya picha,

Man Utd wakiwa na Jose Mourinho walikuwa wameshindwa mara mbili na Chelsea chini ya Conte msimu huu

Meneja wa Manchester United Jose Mourinho amesema vijana wake walifanikiwa "kuwadhibiti" viongozi wa ligi ya England Chelsea na kuwalaza 2-0 Jumapili uwanjani Old Trafford.

Mourinho alikuwa ameumizwa na Chelsea msimu huu mechi za awali tangu ahamie United.

Alikuwa amelazwa 4-0 ligini mechi ya kwanza msimu huu ugenini Stamford Bridge na pia alishindwa robofainali katika Kombe la FA pia uwanjani Stamford Bridge.

Lakini Mreno huyo hakuzidiwa wakati huu ambapo aliwapanga pamoja Marcus Rashford na Jesse Lingard safu ya mshambulizi na akampumzisha Zlatan Ibrahimovic.

Rashford alitangulia kufunga na Ander Herrera, ambaye alimdhibiti vilivyo Eden Hazard ,alifunga la pili kipindi cha pili.

Chanzo cha picha, Reuters

Baada ya mechi, Mourinho alisema "Ni mpango ule ule wa wachezaji 11 ambao ulifanya kazi katika Kombe la FA uwanjani Stamford Bridge. Ndio bora zaidi kwa kucheza kaunta kote nchini na tuliwadhibiti vilivyo.

"Nimefurahishwa sana na vijana wangu. Nina furaha isiyo na kifani - na si kwa sababu ni Chelsea, ni kwa sababu tulihitaji alama hizo tatu.

"Sihisi furaha zaidi kwa sababu ya kulaza Chelsea - tuliwalaza viongozi wa ligi. Haijalishi kama kiongozi wa ligi ni Chelsea au klabu nyingine - tuliwachapa vizuri. Hakuna anaweza kusema hatukufaa kushinda mechi hiyo."

United watakuwa wenyeji wa Anderlecht mechi ya marudiano Europa League Alhamisi, mambo kwa sasa yakiwa 1-1 kutoka kwa mechi ya kwanza.

Watarejea ligini kucheza dhidi ya Burnley Jumapili.

Chelsea nao watakutana na Tottenham nusufainali Kombe la FA Jumamosi ijayo.

Mechi yao ijayo ligini itakuwa nyumbani dhidi ya Southampton.