Mohamed Sissoko kuhamia Mitra Kukar ya Indonesia

Mohamed Sissoko

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Mohamed Sissoko anatarajiwa kuhamia Mitra Kukar

Mabingwa mara tatu wa ligi kuu ya Indonesia Mitra Kukar wametangaza kwamba wameafikiana kuhusu kumnunua mchezaji wa zamani wa Mali, Liverpool, PSG na Valencia Mohamed Sissoko.

Wameamua kumpa nyota huyo mkataba wa mwaka mmoja.

Sissoko, 32, ambaye amewahi kuchezea soka nchini China na India anatarajiwa kujiunga na klabu hiyo baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu.

Akifanikiwa, huenda akachezea Mitra mechi yao ya pili msimu huu ligini dhidi ya PSM nyumbani wikendi ijayo.

Atakuwa mchezaji wa nne wa zamani Ligi ya Premia kuhamia Indonesia baada ya Michael Essien, Carlton Cole na Peter Odemwingie.

Sissoko alichezea Liverpool kati ya 2005 na 2008, na alitekeleza mchango muhimu katika kikosi cha Liverpool kilichoshinda Kombe la FA Uingereza mwaka 2006.

Sissoko alichezea Mali mechi 34 na kuwafungia mabao mawili.

Alicheza michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika miaka 2004, 2008, 2010 na 2013.