Mourinho: Rashford amepita kiwango cha mechi za chini ya miaka 21

Jose Mourinho na Marcus Rashford
Image caption Jose Mourinho na Marcus Rashford

Mkufunzi wa Manchester United Jose Mourinho hadhani kwamba mshambuiaji Marcus Rashford anafaa kuteuliwa katika kikosi cha soka cha wachezaji wasiozidi umri wa miaka 21 katika kuwania ubingwa wa Ulaya.

Raia huyo wa Ureno amesema kuwa wakati mchezaji anapofika kiwango fulani sio vyema kuchezeshwa mechi za chini.

Lakini Mourinho amekiri kwamba shirikisho la soka nchini lina uwezo wa kutoa uamuzi huo.

Rashford mwenye umri wa miaka 19 tayari ameichezea timu ya Uingereza mara nane.

Mchezaji huyo ambaye ameifungia Uingereza mara moja amecheza mechi 49 akiiwakilisha klabu yake na taifa msimu huu, baada ya kufanikiwa kuingia katika kikosi cha kwanza cha United.

Mshambuliaji huyo ana magoli 10 msimu huu, ikiwemo bao la ushindi katika dakika za ziada katika kombe la Yuropa Alhamisi usiku.