Juventus wacheza mechi ya 33 bila kushindwa

Juventus v Genoa Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Genoa hawajashinda mechi hata moja tangu 5 Machi

Viongozi wa Ligi Kuu ya Italia Juventus walilaza Genoa 4-0 na kuendeleza msururu wao wa kutoshindwa nyumbani Serie A hadi mechi 33.

Ezequiel Munoz alijifunga na kuwapa uongozi Juventus dakika ya 17.

Paulo Dybala aliongeza la pili dakika mbili baadaye kabla ya Mario Mandzukic kumbwaga kipa Eugenio Lamanna na kufanya mambo kuwa 3-0 kabla ya muda wa mapumziko.

Leonardo Bonucci alizamisha kabisa jahazi la Genoa kwa kombora la kutoka mbali dakika ya 64, na kuwasaidia Juventus kufungua mwanya wa alama 11 kileleni mwa ligi.

Wapinzani wa karibu wa Juve, Roma watakutana na klabu ya Pescara inayoshika mkia Jumatatu, lakini wana kibarua kuziba pengo kati yao na Juve zikiwa zimesalia mechi tano pekee msimu huu.

Mada zinazohusiana