Arsenal wazima mbio za Manchester United

Arsenal Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mchezaji wa zamani wa United Welbeck alifunga bao la pili

Arsenal walifikisha kikomo mkimbio wa Manchester United wa mechi 25 bila kushindwa kwa kuwalaza mashetani hao wekundu 2-0 mechi ya Ligi Kuu ya England Jumapili.

Ushindi huo uliweka hai matumaini ya Arsenal ya kumaliza katika nafasi nne za kwanza, ingawa bado watatarajia timu nyingine zijikwae.

Mabao ya Arsenal yalifungwa na Granit Xhaka na Danny Welbeck kipindi cha pili.

Jose Mourinho aliwatuma uwanjani Marcus Rashford na Jesse Lingard kujaribu kuokoa timu yake lakini walishindwa kuwakomboa.

Matokeo hayo yamewaacha Arsenal wakiwa nafasi ya sita, alama mbili nyuma ya United ambao wanashikilia nafasi ya tano na sita nyuma ya Manchester City ambao wanashikilia nafasi ya nne.

Hata hivyo, Arsenal wana mechi moja ambayo hawajacheza.

Pamoja na kufufua matumaini ya Arsenal kufuzu kwa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, ushindi huo wa Jumapili pia ulisaidia kufifisha rekodi mbaya ya Wenger dhidi ya Mourinho.

Katika mechi 15 zilizochezwa awali, Wenger hajawahi kuishinda timu iliyokuwa inanolewa na Mourinho, isipokuwa mchezo mmoja tu wakati wa mechi ya Ngao ya Jamii mwaka 2015.

Mourinho alikuwa ameshinda mechi nane, na hizo nyingine saba zikamalizika kwa sare.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Bao la Granit Xhaka liliingia wavuni baada ya mpiga kugonga mgongo wa Ander Herrera

Mourinho alikuwa amefichua awali kwamba angewapumzisha wachezaji wake muhimu, macho yake yakiwa kwenye Europa Ligi ambapo United watacheza mechi ya marudiano nusu fainali wakiwa 1-0 mbele dhidi ya Celta Vigo.

Mourinho anaamini kushinda Europa Ligi ndiyo njia rahisi zaidi kwa United kufuzu kwa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu ujao.

Baada ya kushinda dhidi ya Celta Vigo Alhamisi, United watarejea tena EPL kwa mechi dhidi ya Tottenham Jumapili tarehe 14 Mei.

Arsenal wana mechi ya katikati ya wiki ugenini Southampton Jumatano.

Mada zinazohusiana