Lauren: ‘Msitarajie Wenger ajiuzulu Arsenal’

Beki wa zamani wa Arsenal Lauren Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Lauren alijiunga na Arsenal kutoka Mallorca mwaka 2000 na akawachezea mechi 159 ligini kwa miaka sita

Shinikizo hazitamlazimisha meneja wa muda mrefu wa Arsenal Arsene Wenger ajiuzulu, beki wa zamani wa klabu hiyo Laurena mesema.

Arsenal watakutana na Southampton katika Ligi ya Premia Jumatano jioni na iwapo watashinda huenda wakapanda hadi nafasi ya tano.

Mkataba wa Mfaransa huyo unafikia kikomo mwisho wa msimu huu na amekosolewa sana msimu huu kutokana na matokeo ya klabu hiyo.

Lauren, 40, aliambia BBC Africa: "Anafahamu kukabiliana na presha, natumai kwamba mambo yatakuwa sawa hivi karibuni."

Lauren alichezea Arsenal mechi 159 ligini kati ya 2000 na 2007 na alikuwa kwenye kikosi kinachosifiwa sana cha "invincibles" (Wasioshindwa) ambacho kilishinda taji la ligi mwaka 2003-2004.

Beki huyo wa kulia wa zamani wa Cameroon alisema: "Sidhani (Wenger) atajiuzulu. Amekabiliwa na shinikizo kwa miaka 30-35, akisimamia klabu kubwa zinazokabiliwa na presha."

Februari, Wenger alisema angeamua kuhusu mkataba mpya Machi au Aprili lakini baadaye alisema labda alifanya kosa kwa kuahidi watu kwamba angekuwa ameamua hatima yake katika kipindi hicho.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii