Inter Milan wanamtafuta meneja wa Chelsea Antonio Conte?

Antonio Conte Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Antonio Conte anakaribia kuongoza Chelsea kushinda taji la ligi msimu wake wa kwanza Stamford Bridge

Klabu ya Inter Milan ya Italia imekataa kuzungumzia taarifa kwamba inapanga kuwasilisha ombi kumtaka meneja wa Chelsea Antonio Conte ajiunge nao.

Inter wamemfuta kazi meneja wao Stefano Pioli.

Taarifa nchini Italia zinasema klabu hiyo ya Serie A, inapanga kumuahidi Conte ujira wa £250,000 kwa wiki iwapo ataondoka Chelsea, klabu ambayo ameiongoza kwa msimu mmoja pekee.

Pioli alifutwa kazi Jumanne miezi sita baada yake kuteuliwa kuwa mkufunzi mkuu.

Mkufunzi huyo wa miaka 51 alikuwa amejaza naafsi ya Frank de Boer mwezi Novemba na alikuwa ametia saini mkataba wa kuwa meneja hadi Juni 2018.

Conte, 47, ambaye alikuwa meneja wa timu ya taifa ya Italia, alihudumu kama meneja wa mahasimu wakuu wa Inter, Juventus kati ya 2011 na 2014.

Inter, wakiwa wamesalia na mechi tatu za kucheza msimu huu, wamo nafasi ya saba Serie A, alama tatu nyuma ya AC Milan ambao wanashikilia nafasi ya mwisho ya kufuzu kwa ligi ndogo ya klabu Ulaya, Europa League.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Pioli amewahi kuwa mkufunzi klabu 11 zikiwemo Lazio, Parma na Bologna

Inte Milan hawajashinda mechi hata moja katika mechi saba walizocheza karibuni ligini.Mkufunzi wa timu ya vijana Stefano Vecchi amepewa majukumu ya kuongoza klabu hiyo hadi mwisho wa msimu.

Pioli alikuwa meneja wa tisa Inter tangu kuondoka kwa Jose Mourinho mwaka 2010.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii