Klabu ya wasichana yashinda ligi ya wavulana Uhispania

AEM Lleida Haki miliki ya picha AEM Lleida / Twitter

Timu moja ya soka nchini Uhispania imewashangaza wengi baada ya kuongoza katika livi ya soka ya wavulana.

Hii ni licha ya wengi kutounga mkono soka ya wanawake nchini humo.

Timu hiyo ya AEM Lleida imeangaziwa na gazeti la The New York Times, ambayo waandishi wake walitembea timu hiyo baada ya kushinda ligi ya kanda kwa wachezaji chipukizi eneo la Lleida.

Walishinda ligi kwa kupata ushindi katika mechi 21 kati ya 22 walizocheza.

Nchini Uhispania, timu za wasichana na wavulana huruhusishwa kucheza pamoja hadi wachezaji wanapotimiza umri wa miaka 14.

Timu hiyo ya AEM Lleida imecheza dhidi ya klabu za wavulana tangu 2014.

Hata hivyo, hakukuwa na wadhamini wowote wa timu yoyote ya soka ya wasichana.

Real Madrid, klabu tajiri zaidi Uhispania, haina timu ya wanawake.

"Ili kuwapa wasichana hawa msukumo, tulihisi kwamba walihitaji kucheza dhidi ya wavulana kwa sababu unahitaji wapinzani hatari ndipo uweze kupiga hatua na kujiboresha," Jose Maria Salmeron, mkurugenzi wa AEM Lleida aliambia New York Times.

Alisema wasichana hao pia wamekabiliwa na unyanyapaa na hutukanwa na mashabiki wakati wanapokuwa wanacheza dhidi ya timu za wavulana.

"Ni jambo la kushangaza, lakini matusi mengi sana hutoka kwa kina mama wa wavulana wa timu ambayo tunacheza dhdii yake."

Wamekuwa pia wakiitwa kwa utani "mabinti wa mfalme" na waamuzi wa mechi wakati wa mechi.

Tangu wapate ufanisi wao katika ligi hiyo ndogo ya Lleida, kumeanzishwa kampeni ya kuwachangishia pesa katika mtandao wa Go Fund Me.

Wanatarajia kupata €10,000 (£8,437) za kuwasaidia kulipia mazoezi yao.

"Huwa najaribu kila mara kuonyesha kwamba mchezo wa soka si wa wavulana pekee," mchezaji mmoja kwa jina Andrea Gomez aliambia New York Times.

"Ukiwa mchezaji mzuri kiufundi, pengine unaweza kufidia udhaifu wako wa nguvu mwili."

Hata wavulana ambao walicheza dhidi yao walikiri kwamba walizidiwa.

"Huwa vigumu kushindwa na wasichana," alisema mmoja wa wachezaji wa klabu iliyoshindwa na wasichana hao.

"Lakini hawa ni wachezaji stadi sana."

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii