Wake wa Rais Kagame na Kenyatta Kushiriki mbio Rwanda

Bi Kenyatta akiwa mazoezini Haki miliki ya picha Office of the First lady Kenya
Image caption Wawili hao wanashiriki ikiwa ni mwaka wa 23 wa maadhimisho ya kwibuka

Wake wa marais wa Kenya na Rwanda, Margaret Kenyatta na Jeanette Kagame watashiriki mbio za kimataifa za amani zitakazofanyika mjini Kigali, Jumapili hii.

Wawili hao watashiriki mbio za kilomita saba huku wakiungana na maelfu ya wanariadha na wanadiplomasia.

Mbio hizo za amani zinaingia makala ya 13 mwaka huu huku lengo likiwa ni kusisitiza amani.

Mbali na wawili hao, wanariadha 6000 kutoka mataifa mbalimbali watashiriki katika vitengo vya mbio za masafa marefu za kilomita 42 na 21 mtawalia.

Mbio hizo zitafanyika katika uwanja wa Amahoro, mjini Kigali ambapo mshindi wa mbio za kilomita 41 ataondoka na dola 2400 za marekani naye mshindi wa kilomita 21 akitunukiwa dola 1200 za marekani.

Mkewe Rais Kenyatta amekuwa akishiriki mbio za Beyond zero, zilizofanyika kama kampeni ya kuwasaidia kina mama na watoto wachanga dhidi ya vifo vya mapema.

Rais wa shirikisho la riadha nchini Rwanda, Jean Paul Munyandamutsa amesema kuwa mbio hizo zitatanguliwa na shughuli mbalimbali zitakazowashirikisha watoto na vijana siku ya Jumamosi.

Mashindano ya mwaka huu yanatarajiwa kuwa na ushindani mkali licha ya wanariadha wa Kenya kushinda kwenye makala ya zamani ya mbio hizo ikiwemo mwaka uliopita.

Mada zinazohusiana