Serengeti Boys yatolewa michuano ya U17

Tanzania Haki miliki ya picha Google
Image caption Serengeti Boys

Tanzania imetolewa katika michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 17, baada ya kufungwa 1-0 na Niger katika mchezo wa mwisho wa Kundi B Uwanja wa Port Gentil mjini Gentil, Gabon.

Matokeo hayo yanazifanya Niger na Tanzania zifungane pointi na wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa, hivyo mshindi katika mechi baina yao anafuzu Kombe la Dunia Oktoba mwaka huu India na pia kwenda Nusu Fainali ya michuano hiyo.

Niger anaungana na Mali iliyoongoza kundi kwa pointi zake saba, baada ya ushindi wa mechi mbili na sare moja, wakati Tanzania na Angola zote zinatolewa.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Daniel Laryea wa Ghana, aliyesaidiwa na Seydou Tiama wa Burkina Faso na Attia Amsaad wa Libya, Niger walipata bao lao kipindi cha kwanza, mfungaji Ibrahim Boubacar Marou dakika ya 41 baada ya shambulizi zuri lililowachanganya walinzi wa Serengeti Boys.

Lakini Niger wangetoka uwanjani wanaongoza kwa mabao zaidi baada ya dakika 45 za kipindi cha kwanza kama si umahiri wa kipa Ramadhan Awam Kabwili kuokoa michomo zaidi ya mitatu ya wazi.

Kwa ujumla, Serengeti Boys ilizidiwa mchezo kipindi cha kwanza na kipindi cha pili hali iliendelea kuwa hivyo na hatimaye Niger wakaitoa Tanzania. Wachezaji wa Tanzania walikuwa wenye huzuni baada ya mchezo huku wakilia.

Mbali na Mali na Niger, timu nyingine zilizofuzu Nusu Fainali ni Ghana na Guinea kutoka Kundi A.

Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Ramadhani Kabwili, Ally Ng'anzi, Nickson Kibabage, Dickson Job, Abdul Suleiman, Asad Ali/Muhsin Makame dk85, Kibwana Ally, Shaaban Zuberi, Ally Msengi, Ibrahim Abdallah/Yohanna Nkomola dk46 na Kelvin Naftal.

Niger; Khaled Ibrahim, Yacine Massamba, Habibou Sofiane, Rachid Souley, Abdoul Karim, Djibrilla Ibrahim, Inoussa Amadou, Abdoul Rachid, Ibrahim Boubacar, Ibrahim Namata na Hamid Galissoune Ajina.