Man City wakaribia kumchukua kipa wa Benfica Ederson Moraes

Ederson Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Ederson alisaidia Benfica kushinda Kombe la Ureno mara ya 26 Jumapili kwa kulaza Vitoria Guimaraes 2-1

Manchester City wanakaribia kumnunua kipa wa mabingwa wa ligi ya Ureno Benfica Ederson Moraes kwa jumla ya £33m.

Meneja wa City Pep Guardiola amekuwa akimtafuta mchezaji huyo wa Brazil kwa muda na sasa amepata nafasi baada ya kumwachilia kipa wa klabu hiyo Willy Caballero Ijumaa.

Baada ya ushindi wa 2-1 katika fainali ya Kombe la Ligi nchini Ureno, Moraes alisema kuna uwezekano hiyo ikawa ilikwua mechi yake ya mwisho kuwachezea benfica.

Taarifa zinasema Guardiola pia anataka kumnunua beki wa kati Mfaransa anayechezea Monaco Benjamin Mendy, 22.

Baada ya kukosa kushinda kikombe chochote msimu wake wa kwanza kama meneja City, Guardiol amepanga kufanyia mabadiliko makubwa kikosi cha klabu hiyo kabla ya msimu ujao kuanza.

Pep alichukua hatua ya kwanza wka kumnunua kiungo wa Monaco, Mreno Bernardo Silva kwa £43m Ijumaa.

Caballero ni miongoni mwa wachezaji watano wa City ambao mikataba yao imefikia kikomo na wameruhusiwa kuondoka.

Mshambuliaji Kelechi Iheanacho anatafutwa na West Ham.

Hatima ya wachezaji wanne ambao Guardiola aliwaruhusu waondoke Etihad kwa mkopo msimu uliopita - Joe Hart, Samir Nasri, Wilfried Bony na Eliaquim Mangala - haijabainika

Kuwasili kwa Ederson kutamuongezea presha Claudio Bravo.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii