Afya ya Nahodha wa Simba ,Jonas Mkude yazidi kuimarika

simba Haki miliki ya picha Google
Image caption Jonas Mkude,katikati

Nahodha wa klabu ya soka ya Simba, Jonas Mkude ameruhusiwa kutoka katika hospitali ya Muhimbili, Dar es Salaam alipokuwa amelazwa tangu jana kufuatia ajali ya gari iliyotokea eneo la Dumila mkoani Morogoro.

Mkude na watu wengine watano walikuwa wakisafiri kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam na walipofika Dumila tairi la mbele likapasuka na gari hiyo kupoteza mwelekeo hadi kwenye pori upande wa kushoto.

Abiria mmoja aliyesadikika kuwa ni shabiki wa klabu ya Simba Shoshe Fidelis alifariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa hospitali ya Mkoa wa Morooro, wakati wengine, Jasmin na Faudhia wamelazwa hospitalini hapo, huku dereva ambaye pia ndiye mmiliki wa gari ajulikanaye kwa jina la utani, Rais wa Kibamba anashikiliwa na Polisi.

Mkude alikuwa anatoka Mkoani Dodoma Makao Makuu ya nchi ya Tanzania , ambako juzi aliisaidia Simba kukata tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika mwakani, baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbao FC Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.