Tiger Woods: Sikuwa nimelewa kwa kunywa pombe

Tiger Woods Haki miliki ya picha Alamy
Image caption Police in Palm Beach County, Florida, released a mugshot of the golfer

Mchezaji gofu maarufu duniani Tiger Woods amesema hakuwa amekunywa pombe alipokamatwa akiendesha gari jimbo la Florida mapema Jumatatu.

Mchezaji huyo alifunguliwa mashtaka ya kuendesha gari akiwa amelewa, lakini amesema ulevi wake ulitokana na dawa alizokuwa amezinywa kwa ushauri wa daktari.

"Nafahamu uzito wa kitendo nilichokifanya na nawajibikia kikamilifu vitendo vyangu," amesema.

Polisi walitoa picha ya Bw Woods, akionekana kutokuwa nadhifu, nywele zake zikiwa hazijachanwa na macho akiwa ameyatoa nje na kuonekana mwenye uchovu.

Alikamatwa katika mji wa Jupiter.

"Nataka umma ufahamu kwamba pombe haikuhusika kwa vyovyote vile. Kilichotokea ni madhara ambayo hayakutarajiwa ya kutumia dawa kwa ushauri wa daktari," alisema.

"Sikugundua kwamba kuchanganya dawa kungeniathiri sana hivyo."

Aliongeza: "Ningependa kuomba radhi kwa dhati familia yangu, marafiki na mashabiki. Nilitarajia nifanye vyema kuliko nilivyofanya."


Skabadhi za polisi zinaonesha mwanagofu huyo wa miaka 41 alisimamishwa na polisi mwendo wa saa tisa alfajiri karibu na nyumbani kwake Jupiter na wakamzuilia.

Aliachiliwa huru kutoka gereza la Palm Beach County mwendo wa saa nne unusu asubuhi.

Taarifa zinaonesha aliachiliwa huru "kwa kujitambua mwenyewe", maana kwamba aliahidi kuandika kwamba atashirikiana katika shughuli ya kisheria itakayofuata.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Woods hajashinda taji lolote kubwa duniani katika kipindi cha mwongo mmoja sasa

Woods anaendelea kupata nafuu baada ya kufanyiwa upasuaji wa mgongo.

Akizungumzia afya yake hivi karibuni, alisema upasuaji ulimsaidia kuondoa maumivu makali mgongoni na kwamba hajawahi kujihisi vyema alivyojihisi baada ya upasuaji "katika kipindi cha miaka mingi."

Maisha yake yalianza kuangaziwa sana mwaka 2009 alipokamatwa na kushtakiwa kwa kutomakinika akiendesha gari nje ya nyumba yake Florida.

Alikiri kuwa na uhusiano nje ya ndoa na kuomba radhi hadharani.

Alisema alipokea usaidizi wa wataalamu na kwamba angeendelea kupokea ushauri.

Kutokana na matatizo yaliyomsibu, alipoteza udhamini kutoka wka kampuni nyingi na akachukua likizo pia kutoka kwa mchezo wa gofu kwa muda.

Mada zinazohusiana