Wenger ashauriwa kuwauza Sanchez na Ozil

Kwa pamoja Sanchez na Ozil wamekuwa nguzo muhimu kwa klabu ya Arsenal
Image caption Kwa pamoja Sanchez na Ozil wamekuwa nguzo muhimu kwa klabu ya Arsenal

Mlinzi wa zamani wa klabu ya Arsenal Martin Keown amesema kuwa meneja wa Klabu hiyo Arsene Wenger anapaswa kuwauza nyota wake Alexis Sanchez na Mesut Ozil baada ya kuongeza muda wa kusalia kinoa miamba hiyo ya London.

Mfaransa huyo amesaini mkataba wa miaka miwili na amesema kuwa timu yake inaweza kupigana na kutwaa ubingwa msimu ujao.

Viungo Alexis Sanchez na Mesut Ozil kwa pamoja wanamaliza mikataba yao mwishoni mwa mwaka huu.

Kewon anasema kuliko kupata hasara ya kuwaruhusu kuondoka bure ni vyema akafanya maamuzi magumu ya kuwauza nyota hao na kutengeneza faida itakayoweza kuleta wachezaji wapya na wenye morali kubwa zaidi.

Image caption Wenger ameshinda vikombe vitatu vya ligi na saba vya FA kwa miaka 21 klabuni hapo

Sanchez amefunga magoli 24 na kuchangia kupatikana kwa mengine 10 huku Ozil akifunga nane na kuchangia tisa lakini hiyo haikutosha kuifanya timu hiyo kukosa michuano ya mabingwa wa Ulaya msimu ujao jambo ambalo linatia ukakasi kwa Sanchez na Ozil kuongeza mikataba yao.

Sanchez amepewa ofa ya paundi 300,000 kwa wiki lakini bado hajasaini mkataba huo, huku Ozil akikataa paundi 250,000 kwa wiki.