Antoine Griezmann: Nyota wa Atletico Madrid asema huenda asihamie Manchester

Antoine Griezmann Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Antoine Griezmann akiwa na kikosi cha Ufaransa akijiandaa kwa mechi ya Ijumaa dhidi ya Paraguay

Mshambuliaji wa Atletico Madrid Antoine Griezmann amedokeza kwamba huenda asiihame klabu yake, licha ya kwamba anatafutwa na klabu nyingi kubwa Ulaya ikiwemo Manchester United.

Mfaransa huyo wa miaka 26 aliandika kwenye Twitter: "Sasa zaidi ya zamani! #atleti #alltogether (sote pamoja)."

Alisema hayo saa chache baada ya marufuku ya kuzuia klabu hiyo kununua wachezaji kudumishwa.

Hii ina maana kwamba huenda klabu hiyo isiweze kumnunua mchezaji mwingine iwapo itamuuza.

Mnamo Alhamisi, ilibainika kwamba Manchester United nao pia wanaonekana kupunguza hamu ya kutaka kumnunua.

Kwa kuwa Atletico haiwezi kununua wachezaji wengine hadi Januari, inatarajiwa kwamba Griezmann atapewa mkataba mpua.

United walitaka sana kumnunua mshambuliaji huyo na walikuwa wanatafakari uwezekano wa kufikisha euro 100m (£87m) kumfungua kutoka kwa mkataba wake.

Lakini duru zinasema ununuzi wa Griezmann sasa si kipaumbele kwa United.

Inafahamika kwamba kuumia kwa Zlatan Ibrahimovic kumeifanya klabu hiyo ya Manchester kutafakari upya msimamo wake, kukiwa na wasiwasi kuhusu mkataba wa raia huyo wa Sweden unaomalizika 30 Juni.

Hata akipewa mkataba mpya, hataweza kucheza hadi Januari.

United sasa wanadaiwa kumtafuta mshambuliaji mkuu badala ya mchezaji wa kawaida nambari 10, na wanaamini tayari wana wachezaji wa kutosha kujaza nafasi hiyo.

United wasipompata Griezmann, kuna baadhi wanaosema huenda wakamtafuta Romelu Lukaku wa Everton au Andrea Belotti wa Torino. Wanaweza pia kumtafuta Alvaro Morata wa Real Madrid.

Mada zinazohusiana