Claudio Ranieri apewa kazi ya umeneja Nantes, Ufaransa

Claudio Ranieri Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Meneja mpya wa Nantes, Claudio Ranieri

Meneja wa zamani wa Leicester Claudio Ranieri ni meneja mpya wa klabu ya Nantes, ya Ufaransa.

Klabu hiyo ya Ligue 1 walipewa ruhusa maalum na wasimamizi wa Ligi Kuu ya Ufaransa kumsajili Mtaliano huyo, ikizingatiwa kwamba alitimiza umri wa juu zaidi unaoruhusiwa kwa waamuzi, ambao ni miaka 65.

Ranieri aliwaongoza Leicester City, kujinyakulia taji la klabu bingwa ulaya msimu wa 2015 -16 na kuongeza umaarufu kwa klabu hiyo.

Lakini alipigwa kalamu mwezi Februari, ambapo klabu hiyo ilikuwa ikijipata katika hatari ya kushushwa daraja baada ya kupoteza kwa mfululizo mara tano kwenye ligi.

Ranieri alichukua uongozi baada ya Sergio Conceicao winga wa zamani wa kushoto wa Ureno kuondoka Nantes na kujiunga na Porto.

Conceicao, 42, alichukua uongozi katika klabu hiyo ya Ligue 1 mwezi Desemba mwaka 2016 na kupata ushindi mara nne katika ligi na kumaliza katika nafasi ya saba katika jedwali la timu bora za Ufaransa.

Ranieri ana uzoefu wa kufanya kazi nchini ufaransa, alipoiwezesha Monaco kupandishwa daraja kujiunga na Ligue 1 mwaka 2012 -13 na kuwaongoza kumaliza katika nafasi ya pili nyuma ya Paris St Germain msimu uliofuata kabla ya kuiaga timu hiyo.

Nantes itakuwa timu ya 17 kwa Ranieri kama meneja kwa miaka 31 na ambapo amekuwa mkufunzi pia wa klabu kubwa zaidi za Italia isipokuwa AC Milan.

Atletico Madrid, Chelsea na Valencia ni baadhi ya klabu nyingine ambazo ameziongoza kama meneja nje ya Italia.

Nantes imeshinda taji la Ufaransa mara nane lakini hawajashinda kombe hilo tangu mwaka 2001.

Mada zinazohusiana