Everton wamnunua nahodha wa Ajax Davy Klaassen kwa £23.6m

Davy Klaassen Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Davy Klaassen alikuwa nahodha wa Ajax wakicheza fainali ya Europa League ambapo walishindwa na Manchester United

Klabu ya Everton imekamilisha kumnunua nahodha wa Ajax Davy Klaassen kwa £23.6m ambapo amejiunga nao kwa mkataba wa miaka mitano.

Kiungo huyo wa kati wa Uholanzi wa miaka 24 amechezea Ajax mechi 163, akawafungia mabao 49 tangu alipojiunga nao mwaka 2011.

Alishinda mataji matatu ya Eredivisie akiwa na klabu hiyo.

"Ni vigumu kuondoka Ajax lakini nafikiri ni hatua nzuri kwangu sasa," Klassen ameambia tovuti ya Everton.

Everton walikuwa awali wamenunua kipa Jordan Pickford, 23, kutoka Sunderland kwa £25m, ambayo ni rekodi kwa kipa Mwingereza.

Klaassen amejiunga na Pickford miongoni mwa wachezaji walionunuliwa na klabu hiyo meneja Ronald Koeman anapojaribu kuimarisha kikosi cha klabu hiyo iliyomaliza nafasi ya saba ligini msimu uliopita.

Klabu hiyo itacheza ligi ndogo ya klabu Ulaya, Europa League, msimu ujao.

Toffees pia wanatarajiwa kutumia £16m kumnunua mshambuliaji wa AC Milan M'Baye Niang.

Niang, 22, alikaa msimu uliopita Watford kwa mkopo.

Mada zinazohusiana