Korea Kaskazini yakataa pendekezo la kushirikiana Olimpiki

2018 PyeongChang Januari 26, 2016 Haki miliki ya picha AFP
Image caption Korea Kusini itakuwa mwenyeji wa Michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi mwaka ujao.

Korea Kaskazini imekataa ombi kutoka kwa Korea Kusini kwamba nchi hizo mbili ziunde timu moja kwa ajili ya Michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi mwaka ujao.

Rais mpya wa Korea Kusini Moon Jae-in alikuwa ameunga mkono ushirikiano huo ambao ulipendekezwa na waziri wa michezo Do Jong-hwan.

Lakini mwanachama wa Kamati ya Olimpiki ya Korea Kaskazini (IOC) Chang Un amepuuzilia mbali wazo hilo - na kusema kwamba huu si wakati wa kushauriana kuhusu maafikiano.

Michezo hiyo katika Pyeongchang, Korea Kusini itafanyika kuanzia 9-25 Februari.

Mataifa hayo mawili yamewahi kushirikiana na kuunda timu moja awali - katika mashindano ya ubingwa wa tenisi ya mezani duniani mwaka 1991.

Lakini Bw Chang ameambia vyombo vya habari Korea Kaskazini kwamba: "Ilituchukua vikao 22 vya mazungumzo kuunda timu moja wakati huo...ilituchukua miezi mitano."

"Huo ndio uhalisia tunaokabiliana nao."

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Picha hii ya wanasarakasi wa Korea Kaskazini na Kusini wakipiga picha pamoja Michezo ya Olimpiki mwaka jana ilisambaa sana mtandaoni

Waziri wa michezo wa Korea Kusini alikuwa amependekeza kwamba mataifa hayo yanaweza hata kuunda timu ya pamoja na mchezo wa magongo wa kuteleza kwenye barafu, na hata akapendekeza Kaskazini iwe mwenyeji wa mashindano ya kuteleza kwenye barafu ili kufanya michezo hiyo kuwa michezo ya Olimpiki ya amani.

Rais Moon, hutetea kuwepo kwa mazungumzo na Pyongyang, naye aliunga mkono wazo la ushirikiano zaidi katika Olimpiki.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii