Tetesi za Soka Ulaya Jumatano 28.06.2017 na Salim Kikeke

Alvaro Morata Haki miliki ya picha AFP
Image caption Alvaro Morata

Mchakato wa Manchester United kumsajili mshambuliaji wa Real Madrid Alvaro Morata, 24, unasuasua baada ya Real kupandisha dau la mchezaji huyo hadi karibu pauni milioni 80 (Mirror).

Morata ambaye ameoa hivi karibuni, amelazimika kuondoka kwenye fungate yake ili kuharakisha uhamisho wake kwenda Old Trafford (AS).

Wasiwasi kuhusu hatma ya Cristiano Ronaldo unasababisha kuchelewa kutangazwa kwa uhamisho wa Alvaro Morata kutoka Real Madrid kwenda Manchester United (Diario Gol).

Tottenham wapo tayari kumpa mkataba mpya beki wake Toby Alderweireld, 28, ambaye ananyatiwa na Inter Milan (Daily Mirror).

Mshambuliaji wa Sunderland Jermain Defoe, 34, amekwama kwa sababu Bournemouth na West Ham zinachelea kumchukua kutokana na gharama kubwa za mchezaji huyo (Daily Star).

Mshambuliaji wa Burnley Andre Gray, 26, anataka mkataba mpya wenye mshahara wa pauni 100,000 kwa wiki, lakini klabu hiyo inasema haina uwezo wa kumlipa (Daily Star).

Fernabahce ya Uturuki inafikiria kupanda dau la kumchukua winga wa Everton Kevin Mirallas, 29 (Fanatik).

AC Milan wamejitoa katika mbio za kutaka kumsajili kiungo wa Real Madrid, James Rodriguez, 25, na hivyo kuwapa matumaini zaidi Chelsea na Manchester United (Mundo Deportivo).

Everton wamewazidi kete Manchester United katika kumsajili beki Michael Keane, 24, kutoka Burnley na anatarajiwa kutua Goodison Park siku chache zijazo (Sun).

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Beki wa Arsenal Laurent Koscielny (pili kulia)

AC Milan wanataka kumsajili beki wa kati wa Arsenal, Laurent Koschielny, 31 (Telefoot).

Aston Villa watakamilisha usajili wa beki John Terry, 34, wiki hii ambapo mkataba wake na Chelsea unamalizika (Daily Mirror).

Manchester United bado wataendelea kujaribu kumsajili kiungo wa Monaco Fanbinho, 23, licha ya kumchukua Nemanja Matic, 28, kutoka Chelsea. Jose Mourinho huenda akamchezesha Fabinho kama beki wa kulia (Independent).

Mshambuliaji wa Manchester United Anthony Martial, 21, atamwambia Jose Mourinho kuwa anataka kuondoka, na klabu hiyo haitamzuia kuondoka OT (Daily Express).

Manchester United wamepanda dau la euro milioni 80 kumtaka kiungo wa Real Madrid James Rodriguez (Mediaset Premium).

Francesco Totti, 40, anazungumza na klabu ya Tokyo Verdy kuhusu mkataba wa pauni 50,000 kwa wiki. Totti anaondoka Roma baada ya miaka 25 (Sun).

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Hector Bellerin

Barcelona wamejiwekea makataa ya siku 10 wawe wamemsajili beki wa Arsenal Hector Bellerin na siku hizo zikipita bila kumpata wataelekeza macho yao kwingineko (Mundo Deportivo).

Arsenal wana uhakika Alex Oxlade-Chamberlain atasaini mkataba mpya wa pauni 100,000 kwa wiki, lakini mchezaji huyo anataka kwanza kuhakikishiwa nafasi kabla ya kusaini (Evening Standard).

Zinedine Zidane hana mpango wa kumuuza Gareth Bale msimu huu, licha ya taarifa kuwa Real wanataka kumsajili Kylian Mbappe (Marca).

Beki wa Chelsea Kurt Zouma, 22 huenda akajiunga na Nice kwa mkopo akisaka kucheza katika kikosi cha kwanza (TalkSport).

Kurt Zouma au Michy Batshuayi, mmoja wao huenda akauzwa Sevilla, kama sehemu ya mkataba wa Chelsea kumsajili winga Vitolo (Express).

Manchester United wanataka kumsajili kiungo wa Middlesbrough Marten de Roon, 26, na wanaamini anaweza kupatikana kwa pauni milioni 8.8 (Tutto Mercato).

Chelsea, Tottenham, Everton, Leicester, Southampton na Stoke, zote zinamtaka Ben Gibson, 24, lakini watalazimika kulipa pauni milioni 25 kumpata beki huyo wa Middlesbrough (Daily Star).

Tottenham wanamtaka beki wa Southampton Cedric Soares, 25, lakini wanakabiliwa na upinzani kutoka Barcelona na Juventus (Daily Mirror).

Haki miliki ya picha Reuters

Kiungo wa Leicester Nampalys Mendy, 25, anataka kwenda Bordeaux baada ya kushindwa kucheza vizuri England (L'Equipe).

Barcelona wamekasirishwa na nahodha wao wa zamani Carlos Puyol, baada ya mmoja wa mabeki anaowawakilisha mwenye umri wa miaka 16, Eric Garcia kuamua kuitosa Barcelona na kwenda Manchester City (Independent).

Paris Saint-Germain wanajiandaa kutoa euro milioni 240 kujaribu kuwashawishi Kylian Mbappe na kipa Gianluigi Donnarumma. PSG watatoa euro milioni 135 kwa ajli ya Mbappe na euro milioni 39 kwa ajili ya kipa wa AC Milan Donnarumma, na pia wanataka kutoa euro milioni 42 kumtaka Fabinho wa Monaco na euro milioni 23 kumchukua Raphael Guerrerro kutoka Borussia Dortmund (Sport).

Tianjin Quanjian ya China iko tayari kurejea tena katika mbio za kutaka kumsajili mshambuliaji wa Borussia Dortmund Pierre Emerick-Aubameyang na wapo tayari kutoa euro milioni 80 (SportBild).

Habari zilizothibitishwa tutakujuza mara zitakapothibitishwa. Tetesi nyingine kesho tukijaaliwa. Siku njema.

Mada zinazohusiana