Lionel Messi ajiandaa kufunga ndoa

Antonella Roccuzzo na wana wao wawili waingia uwanjani kuwa na Messi Haki miliki ya picha AFP / Getty Images
Image caption Antonella Roccuzzo na wana wao wawili waingia uwanjani kuwa na Messi

Nyota wa kandanda duniani Lionel Messi atafunga pingu za maisha na mpenzi wake wa tangu utotoni katika mji wake wa kuzaliwa nchini Argentina baadaye leo.

Mchezaji huyo wa Barcelona amerejea katika jiji la Rosario kufunga ndoa na Antonella Roccuzzo, ambaye walikutana kabla yake kuhamia Uhispania akiwa na miaka 13.

Gazeti la Argentina la Clarín limetaja harusi hiyo kuwa "harusi ya mwaka" au hata pengine 2harusi ya karne hii".

Wachezaji wenzake Messi, wakiwemo Luis Suárez na Neymar, watakuwa miongoni mwa wageni 260 watakaohudhuria sherehe hiyo, kwa mujibu wa gazeti hilo.

Wengi wamesafiri huko kwa kutumia ndege za kibinafsi.

Maafisa zaidi wa polisi wametumwa katika mji huo kudumisha usalama katika hoteli wanamokaa, na kampuni ya kibinafsi ya usalama itadumisha ulinzi ndani kuzuia watu wasioalikwa kuingia.

Wanahabari takriban 150 wamepewa idhini ya kuhudhuria ambapo watakaa eneo maalum la wanahabari kwenye ukumbi huo, lakini hawana idhini ya kufika kokote kwenye ukumbi huo, waandalizi wamesema.

Messi na Antonella walikutana wapi?

Haki miliki ya picha AFP / Getty Images
Image caption Mchoraji Lisandro Urteaga akichora picha ya Messi kwenye ukuta kabla ya harusi Rosario kufanyika

Messi, 30, alikutana na mkewe alipokuwa na miaka mitano pekee.

Ni binamuye rafiki yake wa karibu, Lucas Scaglia, ambaye pia ni mchezaji wa kulipwa

Messi alikubali ofa ya kuichezea Barcelona alipokuwa na miaka 13, kwa sharti kwamba wangekuwa wakilipia matibabu yake ya upungufu wa homoni ya ukuaji mwilini.

Amezungumzia changamoto alizokumbana nazo alipolazimika kuwaacha wapendwa wake na klabu yake ya zamani.

Wawili hao, ambao sasa huishi Barcelona, wana wana wawili wa kiume.

Mwezi Mei, rufaa yake dhidi ya kifungo cha miezi 21 jela kwa kukwepa kulipa kodi nchini Uhispania ilikataliwa.

Hata hivyo huenda asiende jela kwani kifungo hicho kinaweza kutumikiwa nje au afidie kwa kulipa faini.

Harusi itakuwaje?

Sherehe ya harusi itafanyika katika hoteli ya City Center, mjini Rosario ambayo pia ina chumba cha kuchezea kamari, yaani casino.

Haki miliki ya picha CityCenter Rosario
Image caption Hoteli ya City Center wakati wa hafla ya awali

Bi Roccuzzo, 29, anatarajiwa kuvaa mavazi kutoka kwa mbunifu wa mavazi Rosa Clara, kutoka Barcelona. Mbunifu huyo amewahi kuwapamba Eva Longoria na Malkia Letizia wa Uhispania.

Nani watahudhuria?

Messi anadaiwa kuwaalika wachezaji wenzake Barcelona, wakiwemo Gerald Piqué na mkewe Shakira.

Wachezaji wenzake timu ya taifa ya Argentina, wakiwemo Sergio Agüero, pia watahudhuria.

Clarín wanasema hajawaalika wakufunzi wake waliopita, akiwemo Pep Guardiola, ambaye sasa yupo Manchester City.

Nyota mwingine wa soka Argentina, Diego Maradona, pia hajaalikwa kwa mujibu wa magazeti Argentina.

Haki miliki ya picha AFP / Getty Images
Image caption Luis Suárez wa Uruguay alipowasili Rosario

Rosario inapatikana wapi?

Mji wa bandarini wa Rosario umo kwenye ukingo wa Paraná, 300km kaskazini magharibi mwa Buenos Aires katikati mwa Argentina.

Mtu mwingine maarufu kutoka Argentine aliyeishi huko utotoni ni Ernesto "Che" Guevara.

Messi hufahamika kwa kifupi tu kama Lío.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Picha Che Guevara karibu na nembo ya klabu ya Newell's Old Boys ukutani

Amekuwa shujaa eneo hilo tangu alipovuma sana akichezea klabu ya eneo hilo ya Newell's Old Boys.

Klabu hiyo ina ushindani mkali na klabu iliyopo karibu ya Rosario Central, uhasama sawa na wa Boca Juniors na River Plate mjini Buenos Aires.

Tangu alipohamia Uhispania, messi ameshinda mataji matano ya Mchezaji Bora Duniani wa mwaka ya Fifa, maarufu kama Fifa Ballon d'Or.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii