Nwankwo Kanu: Kifo cha Tiote chafaa kuwazindua watu

Former Nigeria captain Nwankwo Kanu
Image caption Nwankwo anataka kujenga hospitali za moyo maeneo mbalimbali Afrika

Nyota wa soka wa zamani wa Nigeria Nwankwo Kanu anasema kifo cha hivi majuzi cha mchezaji mashuhuri wa Ivory Coast Cheick Tiote kinafaa kuwa "funzo" na kuhakikisha hatua zinachukuliwa kuhusu maradhi ya moyo barani Afrika.

Tiote, 30, alifariki mapema mwezi huu baada ya kuzirai akifanya mazoezi uwanjani China ambako alikuwa anachezea klabu ya ligi ya daraja la pili ya Beijing Enterprises.

Kanu, ambaye pia alikabiliana na matatizo ya moyo wakati wa uchezaji wake anasema wakati umefika kwa hatua kuchukuliwa kuhusu maradhi ya moyo uwanjani na nje ya uwanja.

Mchezaji huyo wa Nigeria aliacha kucheza kwa miezi tisa baada ya madaktari kugundua kasoro kwenye moyo wake Inter Milan.

Ilikuwa ni miezi kadha baada yake kusaidia taifa lake kushinda dhahabu katika michezo ya Olimpiki 1996 mjini Atlanta.

Hata hivyo, aliweza kurejelea uchezaji wake baada ya kufanyiwa upasuaji Ohio, Marekani.

"Kifo cha Tiote hakikuwa habari nzuri. Haikuwa mara ya kwanza kwa hilo kutokea,2 alisema Kanu, na kuongeza: "Tulimpoteza Marc-Vivien Foe. Alifariki dunia lakini hakuna lililofanywa. Tiote ametutoka na hakuna jambo linalofanywa."

Tiote amejiunga na orodha ndefu ya wachezaji wa Afrika ambao wamefariki uwanjani kutokana na maradhi ya moyo.

Mchezaji huyu wa zamani wa Ajax Amsterdam, Inter Milan, Arsenal na Portsmouth FC anasema atachangia kukabili tatizo hilo.

Anapanga kujenga hospitali ya moyo ya $17 milioni mjini Abuja, Nigeria. Anataka pia kujenga hospitali nyingine kama hiyo katika nchi nyingine za Afrika - moja mashariki, kaskazini na kusini mwa Afrika.

"Nazungumza na marafiki ili tufanye jambo, tuwahamasishe watu, tujaribu kuwasaidia watoto Afrika," anasema Kanu.

"Mtu mmoja hawezi kufanya kila kitu. Kilichomtendekea Tiote ni funzo kwetu sote. Hatuwezi kuruhusu mambo yaendelee hivi. Lazima tulizungumzie. Lazima tuzungumze zaidi kuhusu hili, habari zinafaa kusambazwa kwa sababu tatizo hili ni kubwa."

Suala la maradhi ya moyo Afrika limemshughulisha Kanu sana siku hizi, baada yake kustaafu uchezaji soka.

Ana Wakfu wa Moyo wa Kanu ambao umefanikisha upasuaji wa wagonjwa wa moyo 538 England, India, Nigeria na Israel.

Katika afisi za wakfu huo Lagos, Nigeria kila siku simu kati ya nane na kumi hupigwa kila siku na watu wenye matatizo ya kiafya wanaohitaji usaidizi.

Ili kupata fedha zinazohitajika kujenga hospitali yake Abuja, Kanu amewaleta pamoja marafiki zake katika soka - wachezaji wenzake wa zamani Ajax, Inter Milan, Arsenal na Portsmouth kwa mechi ya kuchangisha pesa ambayo itachezewa Lagos na Johannesburg lbaadaye mwaka huu.

Pesa zitakazochangishwa zitaenda kwa wakfu wake na nyingine kwa Wakfu wa Nelson Mandela.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii