Chelsea yamsajili mlinda lango wa zamani wa Manchester City

Mlinda lango wa zamani wa Manchester City Willy Caballero
Image caption Mlinda lango wa zamani wa Manchester City Willy Caballero

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya England Chelsea, wamemsaini mlinda lango wa zamani wa Manchester City Willy Caballero kwa uhamisho wa bure.

Raia huyo wa Argentina aliachiliwa na City wakati mkataba wake ulipokamilika mwishoni mwa mwezi Juni.

Caballero, 35, aliwasili Uingereza kutoka Malaga mwaka 2014 na alishiriki mechi 26 katika mashindano yote kwa klabu ya Manchester City chini ya mkufunzi Pep Guardiola msimu uliopita.

''Nina furaha sana kujiunga na mabingwa wa Ligi ya Premia,'' alisema. ''Natazamia kukutana na wachezaji hao na kuisaidia klabu hiyo kupata mafanikio zaidi.''

Chelsea ilimuuza mlinda lango wake wa nafasi ya pili Asmir Begovic, 30, kwa Bournemouth mwezi Mei.

Mada zinazohusiana