Afisa wa polisi anayeichezea Black Stars ya Ghana

Samuel Sarfo kushoto ambaye alikuwa mlinzi sasa ni mchezaji mahiri wa Black Stars Haki miliki ya picha SAMUEL SARFO
Image caption Samuel Sarfo kushoto ambaye alikuwa mlinzi sasa ni mchezaji mahiri wa Black Stars

Mwaka mmoja uliopita Samuel Sarfo afisa wa polisi nchini Ghana alipigwa picha , akiwalinda wachezaji wa timu ya soka ya taifa kabla ya mechi ya kimataifa.

Miezi 12 baadaye Sarfo mwenyewe ameichezea The Black Stars kwa mara ya kwanza akiingizwa kama mchezaji wa ziada katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Marekani katika mechi ya kirafiki iliochezwa mjini Connecticut siku ya Jumamosi.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 pia ni nahodha wa klabu ya ligi ya taifa hilo Liberty Proffessionals na anachanganya uchezaji wake wa soka na kazi zake kama afisa wa polisi.

Mengi yamebadilika tangu aonekane na mavazi ya polisi , akilinda kikosi cha taifa na kama alivyomwambia mwandishi wa BBC Afrika Nishat Ladha ana mengi ya kumshukuru mwajiri wake.

Alisema kuwa anatimizi ndoto yake ya kuichezea timu ya taifa.

''Ni ndoto iliotimia.Hiyo ni ndoto ya kila kinda kuvaa jezi za timu ya taifa nchini Ghana''.

Amesema kuwa kiungo wa kati Emmanuel Agyemang-badu ambaye alipiga picha naye akivalia magwanda yake ya polisi na ambaye hakuchaguliwa katika timu hiyo dhidi ya Marekani amekuwa akimsadia sana.

Anasema kuwa anataka kucheza soka ya kulipwa kwa sababu ulimwengu unafaa kuona mchezo wake.

Mada zinazohusiana