Rais wa klabu ajiuzulu kutokana na vitisho vya mashabiki Brazil

Rais wa klabu ya Paysandu Sport ajiuzulu Brazil kutokana na vitisho vya mashabiki Haki miliki ya picha PAYSANDU SPORT
Image caption Rais wa klabu ya Paysandu Sport ajiuzulu Brazil kutokana na vitisho vya mashabiki

Rais wa klabu moja ya soka ya ligi ya daraja la pili nchini Brazil Paysandu Sport amejiuzulu akisema kuwa watu waliojihami wamemtishia kumuua iwapo klabu hiyo itashushwa daraja.

Sergio Serra alisema kuwa alifuatwa akitembea na familia yake na watu waliokuwa katika pikipiki na kutishiwa.

Paysandu ina makao yake huko Belem na ni miongoni mwa kilabu kubwa kaskazini mwa Brazil.

Klabu hiyo imekumbwa na wakati mgumu na iko katika nafasi ya 16 katika ligi ya Serie B ,ikiwa nafasi moja pekee kushushwa daraja.

Christina Serra, dadake Sergio aliripoti katika mitandao ya kijamii kwamba nduguye alikuwa ameenda kujivinjari na mkewe pamoja na watoto siku ya Jumapili.

Mmoja wao ambaye alikuwa ameziba uso wake na shati , alisema kuwa ''Najua unakoishi, Iwapo Paysandu itashushwa daraja hadi Serie C, nitakuua wewe na mkeo na mwanao''.

Ndugu yangu alishituka na akaamua kufanya maamuzi ya kujiuzulu.

Soka ya ya Brazil imekuwa na wakati mgumu kukabiliana na ghasia za mashabiki kwa miongo kadhaa na wachezaji pia wamekuwa wakipokea vitisho.

Mwaka 2011, aliyekuwa beki wa kushoto Robert Carlos alisema kuwa amepokea vitisho vya simu na watu wamekuwa wakilifuata gari lake wakiwa katika pikipiki baada ya klabu yake ya soka Corinthians kubanduliwa katika kombe la Copa Libertadores.