Sudan yapigwa marufuku na Fifa

Fifa badge Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Fifa huzuia serikali kuingilia masuala ya usimamizi wa soka

Shirikisho la soka duniani Fifa limeipiga marufuku Sudan kutokana na serikali ya nchi hiyo kuingilia masuala ya usimamizi wa soka.

Fifa ilikuwa imeionya nchi hiyo baada ya serikali kumteua rais mpya wa Shirikisho la Soka la Sudan.

Marufuku hiyo ina maana kwamba klabu tatu za Sudan zinazocheza katika mashindano ya bara zimeondolewa kwenye michuano hiyo na Shirikisho la Soka la Afrika.

Al Hilal na Al Merreikh hazitaweza kushiriki ligi ya Klabu Bingwa Afrika na pia Al Hilal Obeid haitaweza kushiriki Kombe la Shirikisho.

Hii ina maana kwamba mechi mbili za Ijumaa za mwisho kundi A ambazo zilikuwa zichezwe zikishirikisha Hilal na Merreikh hazitaendelea.

Al Merreikh, ambao walikuwa wanapigania kufika hatua ya muondoano, walipangiwa kukutana na Etoile du Sahel nchini Tunisia leo jioni.

Al Hilal ambao walikuwa tayari hawawezi kusonga walikuwa wanakutana na Ferroviario Beira ya Msumbiji nchini Sudan.

Kutokana na kuondolewa kwa klabu hizo mbili sasa Ferroviario Beira itajiunga na Etoile du Sahel ikatika robofainali Kundi A.

Mechi ya mwisho kundini ya Al Hilal Obeid dhidi ya Zesco United ya Zambia mnamo Jumapili pia imefutiliwa mbali.

Obeid walikuwa tayari wamefuzu kutoka Kundi C lakini sasa, wale ambao walipangiwa kukutana nao robofainali watakutana na Zesco.

Mada zinazohusiana