Taifa Stars yatua Mwanza kujifua

Tanzania Haki miliki ya picha Google
Image caption Taifa Stars

kikosi cha timu ya mpira wa miguu cha Tanzania 'Taifa Stars', kimesafiri kwenda jijini Mwanza kikiwa na ongezeko la wachezaji wapya saba.

Kati ya hao ambao Kocha Mkuu Salum Mayanga amewaita, wamo wale aliowatangaza juma lililopita ambao ni John Bocco, Kevin Sabato pamoja na kinda Athanas Mdamu ambaye anacheza Alliance ya Mwanza inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza.

Katika kikosi chake kabla ya kuivaa Rwanda Jumamosi ijayo, wachezaji wengine ambao Kocha Mayanga amewatangaza leo ni pamoja na Kipa wa Serengeti Boys - timu ya taifa a vijana ya Tanzania, Ramadhan Kabwili.

Mbali ya hao wamo pia Boniface Maganga kutoka Mbao FC, Joseph Mahundi kutoka Azam FC na pia amemrejesha tena Said Ndemla wa Simba SC ambaye awali alikuwa kwenye uangalizi wa majeraha.Kikosi hicho kinakwenda kujiandaa na mchezo dhidi ya Rwanda utakaofanyika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza Jumamosi ya Julai 15, mwaka huu

Kipa Benno Kakolanya, Shaban Idd Chilunda na Mbaraka Yussuf hao wamepumzishwa kwa sababu ya majeraha waliyoyapata kwa nyakati tofauti wakiwa na Taifa Stars huko Afrika Kusini kwenye michuano ya Kombe la Castle la Cosafa - inayoandaliwa na Baraza la Soka kwa nchi za Kusini mwa Afrika.Pia wachezaji wa kimataifa ambao hawahusiki na mechi za CHAN ambao ni Thomas Ulimwengu na Elius Maguri, hawakuongozana na timu.

Timu hiyo ilishika nafasi ya tatu katika michuano ya Castle Cosafa kwa kuishinda Lesotho kwa mapigo 4-2 ya penalti katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Moruleng nchini Afrika Kusini Ijumaa iliyopita.

Taifa Stars inajiandaa na mchezo dhidi ya Rwanda unaotarajiwa kufanyika Jumamosi Julai 15, mwaka huu kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN).

Timu hiyo ambayo kwa mwaka huu imecheza mechi tisa za kimataifa na kushinda mitano; kutoka sare miwili na kufungwa mmoja wa nusu fainali za Cosafa, itakuwa na kikosi cha wachezaji 24.