Michael Carrick achaguliwa nahodha wa Man United

Michael Carrick ndio nahodha mpya wa Manchester United Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Michael Carrick ndio nahodha mpya wa Manchester United

Klabu ya Manchester United imemchagua kiungo wake wa kati Michael Carrick kama nahodha wa klabu hiyo.

Carrick mwenye umri wa miaka 35 ndio mchezaji aliyeichezea Man United kwa kipindi kirefu ,baada ya kujiunga na United 2006 na anachukua mahale pake Wayne Rooney ambaye amehamia klabu ya Everton.

''Nahisi vyema ni fursa kubwa kuiongoza uwanjani timu kama manchester United'' , Carrick aliiambia MUTV.

''Sikudhania kwamba nitasalia katika klabu hii kwa muda huu mrefu na kufanikiwa hivi .Nimekuwa nikiipenda klabu hiii na kuwa katika nafasi kama hii ni kitu maalum kwangu''.

Aliongezea: Nitazungumza wakati ninapohitaji kuzungumza,lakini mimi hupenda kunyamaza na kutulia.Nitajaribu kuiongoza timu hii na kuwa mfano mwema.

Carrick alijiunga na United kutoka Tottenham kwa pauni milioni 18.6 na kuongeza kandarasi yake mwaka huu hadi 2018.

Ameichezea klabu hiyo mara 459 , kushinda kombe la ligi mara 5 ,kombe la FA na lile la vilabu bingwa Ulaya.