Arsenal yailaza Bayern Munich nchini China

Arsene Wenger Haki miliki ya picha Getty Images

Klabu ya Arsenal inayocheza Ligi Kuu ya England imeandikisha ushindi wa jumla ya 4-3 kupitia mikwaju ya penalti dhidi ya miamba wa Ujerumani Bayern Munich.

Walipata ushindi huo kwenye mechi ya kirafiki iliyochezewa mjini Shanghai, China.

Mechi ilikuwa imemalizika 1-1 muda wa kawaida.

Bao la Bayern lilifungwa na Lewandowski mapema dakika ya 9 kupitia mkwaju wa penalti baada ya Maitland-Niles kumchezea visivyo mchezaji wa Bayern Bernat.

Arsenal walisawazisha kwa kichwa kupitia Alex Iwobi aliyefunga baada ya kupokea krosi kutoka kwa Aaron Ramsey dakika ya 90.

Kwenye matuta, Alaba alizuiwa kufunga mkwaju wa kwanza wa Bayern na kipa Emi Martinez lakini Ramsey akafunga.

Hummels alifunga lakini Elnenny akashindwa baada ya mkwaju wake kudakwa.

Msururu uliofuata, Coman alifungia Bayern naye Monreal akafungia Arsenal.

Sanches naye alishindwa kufungia Bayern lakini Iwobi akatikisa wavu.

Bernat kisha alishindwa kufunga baada ya Emi Martinez kunyaka mpira wake na kukabidhi Arsenal ushindi.

Ni habari njema kiasi kwa Arsenal, ambao katika michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu uliopita, walilazwa jumla ya 10-2.

Mada zinazohusiana