Beki wa Manchester United Phil Jones apigwa marufuku kwa kumtusi afisa wa Uefa

Phil Jones Haki miliki ya picha Getty Images

Beki wa Manchester United Phil Jones amesimamishwa kucheza mechi mbili za Ulaya kwa kumtusi afisa wa kukabiliana na matumizi ya dawa za kutitimua misuli michezo wa shirikisho la soka Ulaya, Uefa wakati wa fainali ya kombe la ligi ndogo ya klabu Ulaya, Europa League.

Jones amepatikana na hatia ya "kuelekeza matusi na kwa kutoa maneno ya matusi" na kwa "kutoonesha ushirikiano na heshima" kwa afisa huyo.

United pia wametozwa faini £8,900, naye beki Jones, 25, amepigwa faini £4,450.

Mchezaji mwenzake Daley Blind pia ameshtakiwa kwa kukiuka sheria za kukabiliana na matumzii ya dawa zilizoharimishwa, lakini ametozwa faini £4,450.

Inadaiwa Jones alikasirika kwa sababu afisa huyo alikataa kumruhusu akapigwe picha na wachezaji wengine wa United waliokuwa wanainua bango la kutoa heshima kwa waathiriwa wa shambulio la Manchester la 22 Mei.

United walilaza Ajax 2-0.

Jones alikuwa benchi na hakuchezeshwa katika mechi hiyo.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Jones alikuwa kwenye benchi fainali ya Europa League mjini Stockholm, ambapo United walilaza Ajax 2-0

Sasa, hataweza kucheza mechi ya Super Cup ya Uefa dhidi ya Real Madrid mnamo 8 Agosti Skopje.

Aidha, atakosa mechi ya kwanza hatua ya makundi katika Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

Mada zinazohusiana