Diego Costa asema Chelsea wanamchukulia kama 'mhalifu'

Diego Costa

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Costa alifunga mabao 20 katika mechi 35 alizochezea Chelsea na kuwasaidia kushinda ligi msimu uliopita

Diego Costa amesema Chelsea wamekuwa wakimchukulia kama "mhalifu" na akathibitisha kwamba bado anataka kurejea Atletico Madrid.

Mshambuliaji huyo wa miaka 28 alichezea Chelsea mara ya mwisho fainali ya Kombe la FA mwezi Mei na mwezi Juni alitumiwa ujumbe wa simu na meneja Antonio Conte kumfahamisha kwamba hakuwa kwenye mipango yake ya msimu ulioanza siku chache zilizopita.

Costa amesema sasa klabu hiyo inamshurutisha kurejea akafanye mazoezi na wachezaji wa akiba.

"Ni kwa nini hawataki kuniacha niondoke iwapo hawanitaki?" aliambia Daily Mail.

"Lazima nifanye yale inanibidi kuyafanya. Lazima nifikirie kuhsuu maslahi yangu. Nimekuwa mvulana mzuri hapa na nilijaribu kufanya kila kitu sawa. Mapenzi yangu ni kwenda Atletico."

Costa anaamini kwamba meneja Antonio Conte ndiye anayemchongea.

"Januari, mambo yalifanyika kati yangu na kocha. Nilikuwa nimekaribia sana kutia saini mkataba mpya lakini akasimamisha hilo. Nashuku meneja alihusika. Aliomba hilo lifanyike.

"Mawazo yake ni wazi na hayabadiliki. Nimeona yeye ni mtu wa aina gani. Ana mtazamo wake na huo hautabadilika.

"Namheshimu sana kama kocha. Amefanya kazi nzuri na naona hilo, lakini kama binadamu, la. Si mkufunzi ambaye ana uhusiano wa karibu na wachezaji. Hukaa mbali. Hana sifa za kuhusiana vyema na wachezaji.

Juni, Costa alitumiwa arafa na Conte kufahamishwa hangekuwa kwenye mipango ya timu.

"Sijaufuta ujumbe huo wa simu. Watu wakinituhumu kwamba nasema uongo, naweza kuwaonesha. Ujumbe huo ulikuwa wazi, alisema simo kwenye mipango yake na akanitakia kila la kheri siku zijazo. Weka kikomo hapo."

Mshambuliaji huyo wa Uhispania alipewa muda zaidi kupumzika na Chelsea mwezi jana lakini sasa anasema anaadhibiwa kwa hilo.

Anasema anatozwa faini kwa kutokuwa kwenye klabu muda huo na amesema anafikiria kwenda kortini au kujaribu kumaliza sehemu iliyosalia ya mkataba wake bila ujira nchini Brazil.

"Unajua meneja hanitaki," aliongeza Conte.

"Nasubiri Chelsea waniachilie huru. Sitaki kuondoka. Nilikuwa na furaha. meneja asipokutana, ni lazima uondoke."

Costa ambaye ni mzaliwa wa Brazil lakini huchezea timu ya taifa ya Uhispania alijiunga na Chelsea kutoka Atletico Madrid kwa £32m mwaka 2014.

Alikaa misimu minne Atletico na alikuwa amedokeza kwamba huenda akarejea katika klabu hiyo.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Costa alifunga mabao 22 katika mechi 42 mashindano yote msimu uliomalizika majuzi

Lakini klabu hiyo ya La Liga imepigwa marufuku kununua wachezaji hadi Januari.

"Kukaa miezi mitano bila kucheza? Sijui, ni kizungumkuti, lakini watu wanajua kwamba naipenda sana Atletico na kwamba huwa napenda kukaa Madrid," Costa alisema mwezi Juni.

Januari, Costa aliachwa nje ya kikosi cha Chelsea kilichosafiri kucheza mechi ugenini Leicester baada yake kukorofishana na mkufunzi wa mazoezi.

Hilo lilitokea baada ya kuibuka kwa taarifa kwamba alikuwa amepata ofa kutoka China ya kulipwa mshahara wa £30m kwa mwaka. Wakati huo, Chelsea walisema hawakuwa na nia ya kumuuza.

Baadaye Januari, mmiliki wa Tianjin Quanjian alisema juhudi zao za kutaka kumnunua Costa zilitatizwa na sheria mpya kuhusu wachezaji wa kutoka nje Ligi Kuu ya Uchina.

Kuanzia msimu ujao, klabu za Uchina zinaruhusiwa kuchezesha wachezaji watatu pekee kutoka nje ya nchi kwenye mechi badala ya wanne kama ilivyokuwa awali.