Mo Farah ashinda mbio zake za mwisho uwanjani Zurich

Mo Farah Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mo Farah alihimili ushindani mkali kutoka kwa Muktar Edris aliyemshinda katika mbio za 5,000m London 2017

Bingwa wa riadha wa Uingereza Mo Farah aliaga tasnia ya riadha za uwanjani kwa ushindi katika mbio zenye ushindani mkali za 5,000m za Diamond League mjini Zurich.

Farah mwenye umri wa miaka 34, ambaye ameshinda mataji manne ya Olimpiki, sasa ataangazia mbio za nje ya uwanja.

Alikabiliwa na ushindani mkali sana mita 100 za mwisho na bingwa mpya wa dunia kutoka Ethiopia Muktar Edris lakinia akashinda kwa muda wa dakika 13 na sekunde 06.05.

Mmarekani Paul Chelimo alimaliza wa pili baada ya Edris, aliyemshinda Farah katika mbio za London 2017, kuanguka akipiga mbizi kujaribu kuvuka mstari wa mwisho.

Farah alishinda dhahabu katika mbio za 10,000m katika mashindano ya ubingwa wa dunia wa riadha duniani mwezi huu kabla ya kupoteza taji lake la mbio za 5,000m katika mashindano hayo.

Hata hivyo, alishinda mbio zake za mwisho uwanjani akiwa Uingereza zilizofanyika mjini Birmingham.

"Nilitaka kushinda, na nina furaha sana, lakini ilinilazimu kutoa jasho sana. Nitakosa sana mbio za uwanjani, watu, na mashabiki."

Mbio za 5,000m zilikuwa miongoni mwa mataji 16 ya Diamond League yanayoshindaniwa Zurich.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii