Kampuni ya mwana wa Abeid Karume yakumbwa na mlipuko Tanzania

Wakili Fatma Amani Abeid Karume ni mwana wa aliyekuwa rais wa Zanzibar Amani Abeid Karume Haki miliki ya picha Facebook
Image caption Wakili Fatma Amani Abeid Karume ni mwana wa aliyekuwa rais wa Zanzibar Amani Abeid Karume

Makao makuu ya kampuni ya mawakili inayomilikiwa na wakili maarufu pamoja na mwana wa kike wa aliyekuwa rais wa Zanzibar Amani Abeid karume, Bi Fatma Karume mapema Jumamosi alfajiri yalikumbwa na mlipuko wa bomu.

Kampuni hiyo inaorodhesha kampuni za mawasiliano, kawi, benki pamoja na serikali kama mojawapo ya wateja wake.

Wakili Karume hivi karibuni amekuwa akimwakilisha kiranja wa upinzani bungeni Tundu Lissu mahakamani kwa mashtaka ya kuitusi serikali.

Bwana Lissu amekana mashtaka hayo.

Wakaazi wa eneo hilo katikati mwa mji wa Dar es Salaam wanasema walisikia misururu ya milipuko mikubwa muda wa saa nane alfajiri na muda mchache baadaye jumba hilo likajaa moshi na vifusi.

Mashahidi wengine wamesema kuwa walipata kifaa cha bomu la bomba.

Lakini maafisa wa polisi wamesema kuwa ni mapema mno kusema kuwa lilikuwa shambulio la bomu.

Mmoja ya mawakili wa kampuni hiyo amesema kuwa afisi yao iliharibiwa lakini hakuna kilichoibwa.

Rais wa chama cha mawakili wa Tanganyika Tundu Lissu ameshutumu shambulio hilo kama shambulio dhidi ya uhuru wa mawakili.