Man City yailaza Bournemouth, Sterling apewa kadi nyekundu

Gabriel Jesus kulia baada ya kusawazisha dhidi ya Bournemouth Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Gabriel Jesus kulia baada ya kusawazisha dhidi ya Bournemouth

Meneja wa klabu ya Manchester City Pep Guardiola anataka kuelezwa ni kwa nini Raheem Sterling alipewa kadi nyekundi baada ya kufunga bao la ushindi kunako dakika ya 97 dhidi ya Bournemouth.

Baada ya kufunga bao hilo Sterling alikimbia hadi walipo mashabiki wa City na kuanza kusherehekea nao hatua ilioshinikiza refa Mike Dean kumpatia kadi ya pili nyekundu.

''Sielewi. Natumai watanipigia simu kunielezea sababu iliosababisha Sterling kutolewa nje'', alisema Guardiola.

Gabriel Jesus alikuwa ameisawazishia City baada ya Charlie Daniels kuiweka kifua mbele Bournemouth.

Timu hiyo ya nyumbani ilitawala mchezo mapema na kuchukua uongozi baada ya dakika 13 wakati Daniels alipotamba na mpira na kupiga mkwaju mkali ambao ulimwacha kipa bila jibu.

Lakini City ilisawazisha dakika nane baadaye wakati David Silva alipomwekea Jesus pasi nzuri ambapo mchezaji huyo wa Brazil alicheka na wavu.