Asensio awika sare ya Real Madrid na Valencia

Marco Asensio Haki miliki ya picha Getty Images

Marco Asensio alifungia Real Madrid mabao mawili katika mechi waliyotoka sare ya 2-2 na Valencia Jumapili.

Asensio mwenye miaka 21 alifungua ukurasa wa mabao kwa kufunga bao akiwa hatua 20 kutoka kwenye goli.

Carlos Soler alisawazisha na Geoffrey Kondogbia akawaweka Valencia kifua mbele kabla ya Asensio kusawazisha kupitia mkwaju wa ikabu.

Karim Benzema - aliyepoteza nafasi nyingi nzuri - nusura awashindie Real mechi hiyo lakini mpira wake wa kichwa ulifikiwa na kipa Neto baada ya kufanya kazi ya ziada.

Real, ambao walikuwa bila mshambuliaji wao Cristiano Ronaldo aliyepigwa marufuku, walimchezesha kiungo wa kati Casemiro safu ya ulinzi kwani Sergio Ramos bado anatumikia marufuku.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Marco Asensio amefunga mabao manne katika mechi tano mashindano yote msimu huu

Mabeki wao wengine Raphael Varane na Jesus Vallejo wanauguza majeraha.

Kondogbia walikuwa akichezea Valencia mara yake ya kwanza pamoja na Jeison Murillo, baada ya wawili hao kujiunga na klabu hiyo kwa mkopo kutoka Inter Milan wiki hii.

Sare hiyo ya Jumapili iliwakosesha Real na Valencia nafasi ya kujiunga na Real Sociedad, Barcelona na Leganes walio na alama sita kileleni baada ya mechi mbili za kwanza kuchezwa.

Mada zinazohusiana