Beki wa Arsenal Kieran Gibbs kwenda West Brom

Kieran Gibbs Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Kieran Gibbs alicheza mechi 11 Ligi ya Premia msimu uliopita

West Brom wanakaribia kukamilisha ununuzi wa beki wa kushoto wa Arsenal Kieran Gibbs.

Klabu hizo mbili zimeafikiana ada ya £5m kwa mchezaji huyo wa miaka 27 ambaye pia alikuwa akifanya mashauriano na Watford pamoja na klabu ya Galatasaray ya uturuki.

Gibbs bado atahitajika kufanyiwa uchunguzi wa matibabu kabla ya kutia saini mkataba wake.

Kwingineko, Arsenal wamejiunga na Manchester City na Leicester City katika kutaka kumsajili beki wa kati wa West Brom Jonny Evans.

Evans ataruhusiwa kuondoka Hawthorns iwapo tu West brom watafanikiwa kupata mchezaji wa kujaza pengo atakaloacha.

Wanamtaka zaidi mchezaji wa Manchester City Eliaquim Mangala na iwapo Manchester City watamtaka kwa kweli Evans, basi uhamisho huo utakuwa rahisi.

Hata hivyo, Mangala angependa zaidi kujiunga na Inter Milan.

Inter nao zaidi wanataka kumchukua mchezaji wa Arsenal Shkodran Mustafi.

Lakini nao Gunners watakubali tu kumuuza Mustafi iwapo watapata mchezaji wa kujaza pengo atakaloacha, na mchezaji wanayedhani anaweza kufanya hivyo vyema zaidi ni Evans.

West Brom pia wanaweza kufikiria kumnunua nyota wa Liverpool Mamadou Sakho, lakini huenda wakatatizika kufikisha ada yake na mshahara wake.

Mada zinazohusiana