Drinkwater aomba kuondoka Leicester City

Danny Drinkwater Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Danny Drinkwater alichezea Leicester mechi 35 na kuwasaidia kushinda Ligi ya Premia 2015-16

Kiungo wa kati wa Leicester City Danny Drinkwater ameomba kuondoka klabu hiyo huku Chelsea wakiendelea kumtafuta.

Mabingwa hao wa Ligi ya Premia wamewasilisha dau mara mbili bila mafanikio kutaka kumchukua mchezaji huyo wa England ambaye aliongeza mkataba wake wa kumuweka katika Leicester hadi 2021 majira ya joto yaliyopita.

Leicester wamekuwa wakisisitiza kwamba hawataki kumwachilia Drinkwater, 27, ambaye alikuwa sehemu muhimu katika kikosi chao kilichoshinda ligi mwaka 2016.

Meneja wa Chelsea Antonio Conte hata hivyo anataka mchezaji wa kujaza nafasi iliyoachwa na Nemanja Matic.

Drinkwater alicheza mechi 35 kati ya 38 walizocheza Leicester msimu ambao walishinda ligi na alikuwa na ushirikiano wa kufana sana safu ya kati na N'Golo Kante, aliyejiunga na Chelsea Julai mwaka jana.

Bado hajachezeshwa msimu huu kutokana na jeraha la paja.

Drinkwater alijiunga na Leicester mwaka 2012 kutoka Manchester United, na amechezea timu ya taifa ya England mara tatu tangu Machi 2016.

Mada zinazohusiana