Liverpool waanza mazungumzo kuhusu Oxlade-Chamberlain

Alex Oxlade-Chamberlain Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Alex Oxlade-Chamberlain alianza kwenye mechi ambayo Arsenal walishindwa Anfield Jumapili

Liverpool wameanza mazungumzo na Arsenal kuhusu uhamisho wa kiungo wa kati Alex Oxlade-Chamberlain.

Mchezaji huyo wa miaka 24 alikataa kuhamia Chelsea Jumanne hata baada ya klabu hizo kuafikiana kuhusu uhamisho wake wa £40m.

Oxlade-Chamberlain anayechezea timu ya taifa ya England anataka kucheza kama kiungo katika safu ya kati na anahisi kwamba anaweza akapata nafasi Anfield.

Alikataa kuhamia Chelsea baada ya kugundua kwamba huenda wakataka kumtumia katika upande wa kushoto uwanjani.

Bado haijabainika iwapo Liverpool watafikia dau ambayo Chelsea walikuwa wamewasilisha.

Oxlade-Chamberlain anatumikia mkataba wake wa mwisho Emirates na amechezea mechi zote nne za Arsenal msimu huu licha yake kumwambia meneja Arsene Wenger kwamba hatatia saini mkataba mpya.

Alishangiliwa na wachezaji wa Liverpool alipoondolewa uwanjani wakati wa mechi ya Jumapili ambayo Arsenal walilazwa 4-0 uwanjani Anfield Jumapili.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Alex Oxlade-Chamberlain alijiunga na Arsenal Agosti 2011

Kiungo huyo wa kati amechezea Arsenal mechi 198 tangu ajiunge nao kutoka Southampton Agosti 2011.

Liverpool wamekuwa wakimtafuta winga wa Monaco Thomas Lemar ambaye bei yake inakadiriwa kuwa £75m lakini hawatarajiwi kuwanunua wachezaji hao wawili.

Mada zinazohusiana