Tottenham kumnunua Serge Aurier kutoka PSG

Serge Aurier Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Serge Aurier amechezea Ivory Coast mechi 41

Tottenham wanatarajiwa kukamilisha ununuzi wa beki wa Paris St-Germain Serge Aurier baadaye leo Alhamisi.

Mkataba wa uhamisho wake wa karibu £23m umecheleweshwa na matakwa kuhusu kibali cha kufanyia kazi Uingereza.

Changamoto zilizuka kwa sababu mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Ivory Coast mwenye miaka 24 ana hukumu iliyoahirishwa kwa sababu ya kosa la kumshambulia afisa wa polisi mjini Paris mwaka jana.

Hata hivyo, taarifa zinasema tatizo hilo limetatuliwa na Spurs wanaweza kuendelea na utaratibu wa kumchukua beki huyo wa kulia.

Atakuwa mchezaji wa nne kununuliwa na Spurs majira ya sasa ya joto, baada ya beki Juan Foyth, golikipa Paulo Gazzaniga na beki wa kati Davinson Sanchez aliyenunuliwa kwa rekodi ya klabu hiyo ya £42.

Kyle Walker, 27, aliuzwa Manchester City kwa £50m mwezi Julai naye beki wao Kevin Wimmer akajiunga na Stoke City kwa £18m.

Aurier alijiunga na PSG kutoka Toulouse, awali kwa mkopo mwaka 2014, kabla ya kuhamia Paris kwa mkataba wa kudumu mwaka 2015.

Ameshinda mataji mawili ya ligi Ufaransa na vikombe viwili vya ligi.

Alianza kila mechi timu ya taifa ya Ivory Coast iliposhinda Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2015, ambapo alifunga mkwaju wa penalti wakati wa matuta dhidi ya ghana kwenye fainali.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Aurier alishinda Kombe la Mataifa ya Afrika akiwa na Ivory Coast mwaka 2015

Auries alihukumiwa kifungo cha miezi miwili ambacho kiliahirishwa na alizuiwa kuingia Uingereza Novemba mwaka 2016 kabla ya mechi ya PSG dhidi ya Arsenal katika Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

Mada zinazohusiana