Liverpool wamsajili Alex Oxlade-Chamberlain kwa £35m kutoka Arsenal

Alex Oxlade-Chamberlain Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Alex Oxlade-Chamberlain alijiunga na Arsenal kutoka Southampton Agosti 2011

Liverpool wamekamilisha usajili wa kiungo wa kati wa England Alex Oxlade-Chamberlain kutoka Arsenal kwa kulipa £35m.

Mchezaji huyo wa miaka 24 alikataa kuhamia Chelsea Jumanne hata baada ya klabu hizo mbili kuafikiana.

Ametia saini mkataba wa miaka mitano ambapo atakuwa akilipwa £120,000 kila wiki.

Oxlade-Chamberlain, aliyekuwa anatumikia mwaka wake wa mwisho katika mkataba wake Arsenal, alikataa mkataba mpya ambapo angekuwa akilipwa hadi £180,000 kila wiki Emirates.

Oxlade Chamberlain amecheza kila mechi ya Arsenal kufikia sasa msimu huu ikiwemo kichapo cha 4-0 ilichopata Arsenal dhidi ya Liverpool Jumapili.

Kiungo huyo wa kati amechezea Arsenal mechi 198 tangu ajiunge nao kutoka Southampton Agosti 2011, ambapo amewafungia mabao 20.

Alishangiliwa na wachezaji wa Liverpool alipoondolewa uwanjani wakati wa mechi ya Jumapili ambayo Arsenal walilazwa 4-0 uwanjani Anfield Jumapili.

"Najua chaguo langu huenda likawashangaza wengi, na uamuzi wa kuondoka ulikuwa mgumu baada ya kuwa kwenye klabu hii kwa miaka mingi hivyo, lakini nahisi kwamba ndiyo hatua sahihi kwangu katika hatua nyingine ya kujiboresha," amesema kwenye Instagram.

Meneja wa Liverpool Jurgen Klopp amesema anafurahia sana kumpata mchezaji mzuri hiyo na mwenye kipaji.

Amesema hata hakufikiria mara mbili kumnunua.

Hayo yakijiri, mshambuliaji wa Ubelgiji Divock Origi ambaye amekuwa Liverpool amekamilisha kuhamia klabu ya Wolfsburg ya Ujerumani kwa mkopo wa msimu mmoja.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Alex Oxlade-Chamberlain akichezea Arsenal dhidi ya Liverpool uwanjani Anfield

Mchezaji huyo wa miaka 22 alifunga mabao 21 katika mechi 77 alizowachezea Liverpool.

Wakati huu, Liverpool wamewanunua winga Mohamed Salah kutoka Roma kwa £34m, mkabaji kamili Andrew Robertson kutoka Hull kwa £8m na mshambuliaji Dominic Solanke baada ya mkataba wake Chelsea kufika kikomo.

Mshambuliaji wao wa Brazil Philippe Coutinho bado anatafutwa na Barcelona.

Wachezaji wengine wa zamani wa Southampton waliohamia Liverpool:
Nathaniel Clyne (Southampton kwenda Liverpool, Julai 2015m, £12.5m)
Dejan Lovren (Southampton kwenda Liverpool, Julai 2014, £20m)
Sadio Mane (Southampton kwenda Liverpool, Julai 2016, £34m)
Adam Lallana (Southampton kwenda Liverpool, Julai 2014, £25m)

Mada zinazohusiana